Na Dotto Mwaibale
MKUU wa Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, Felix Lyaviva amewashauri wanafunzi waliopo shuleni kujiandaa kujiajiri na siyo kuajiriwa baada ya kuhitimu masomo yao.
Lyaviva ametoa rai hiyo leo alipokuwa akifunga mafunzo ya ukakamavu ya wanafunzi wa Kidato cha Tano 2018 wa Shule ya Sekondari ya Jitegemee ya jijini Dar es Salaam.
Akiwahutubia wanafunzi hao mbele ya wazazi, walimu, maafisa wa jeshi wakiwemo wastaafu na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla hiyo, Lyaviva alisema; "Nawapongeza sana kwa mafunzo ya ukakamavu mliyopewa, mmeonesha ni jinsi gani mlivyoiva lakini niwaombe muwe na ndoto za kujiajiri siyo kuajiriwa mara mtakapotoka hapa."
Mkuu huyo wa wilaya, amewaasa wanafunzi kutojihusisha na vitendo vya mapenzi, uvutaji wa madawa ya kulevya na sigara ambavyo vinaathari kubwa katika maisha.
"Nyie wanafunzi wa kike, nawaasa msikubali kurubuniwa na wenzetu wa kiume kwani athari zake ni kupewa mimba ambazo zitawaharibia maisha yenu huku wao wakiendelea na masomo," alisema Lyaviva.
Aliongeza kuwa, ni vyema wanapotongozwa wakatoa taarifa kwa walimu wa nidhamu ili vijana wenye tabia hiyo washughulikiwe na siyo kuwachekea.
Kuhusu suala la kujiajiri, aliwashauri wanafunzi wawaeleze wazazi wao nini wanapenda kufanya maishani mwao ili wazazi wawaunge mkono kwa kuwaandalia mazingira ya kutimiza ndoto zao hizo.
"Kama unapenda kumiliki shule ya awali, wape wazo lako wazazi wako ambao wanaweza kukuunga mkono kwa kukujengea darasa moja halafu hapo baadaye ukaendelea mwenyewe, msiwaze kabisa suala la kuajiriwa," alisema.
Aliongeza kuwa, hawawezi kutimiza ndoto zao kama hawatakuwa na hofu ya Mungu na kuzifuata amri zake kumi ambazo zipo kwenye vitabu vyote vitakatifu.
"Mkisoma kwa bidii huku mkiwa na hofu ya Mungu na kutimiza amri zake kumi, mtafanikiwa maishani mwenu, lakini mkienda kinyume mtakwama," alisema mkuu huyo wa wilaya.
Mwalimu mkuu wa shule hiyo, Kanali Robert Kessy akimkaribisha Lyaviva aliyekuwa mgeni rasmi, alimshukuru kwa kukubali kufika kufunga mafunzo hayo.
Kessy alimfahamisha mkuu huyo dhumuni la mafunzo hayo kwa wanafunzi kwamba ni kuwaweka katika hali ya ukakamu, kuwa na nidhamu, afya nzuri na kuwa wazalendo kwa nchi yao.
"Mafunzo haya yalianza rasmi mwaka 1985 yalikuwa ya wiki mbili na yaliongozwa na makamanda wetu, lakini ilipofika mwaka 2003 ndipo wanafunzi walipoanza kujiongoza wenyewe kama unavyoona," alisema Kessy.
Gwaride hilo lililowahusisha wanafunzi wa kiume na wakike lilikuwa na vikosi nane pamoja na kikosi maalum cha ukakamavu 'komandoo' liliongozwa na Stanrey Emmanuel.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva akiwasili kwenye uwanja lilipofanyika gwaride la wanafunzi. (kulia) ni Mkuu wa Shule ya Sekondari Jitegemee, Robert Kessy. |
Kamanda mkuu wa gwaride, Stanrey Emmanuel akikabidhiwa zawadi na Mkuu wa Wiyala ya Temeke, Felix Lyaviva kwa kuliongoza vizuri gwaride hilo. |
Wimbo wa Taifa ukiimbwa.
Wazazi na walezi wa wanafunzi hao wakifuatilia gwaride hilo.
Kikosi cha nne kikitoa heshima kwa mgeni rasmi kilipokuwa kikitembea kwa mwendo wa haraka.
Gwaride la ukakamavu likipita mbele ya mgeni rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva akimkabidhi zawadi Julieth Peter aliyekuwa kamanda wa kikosi namba tatu kwa kuongoza vizuri kikosi chake.
Mkuu wa shule ya Sekondari ya Jitegemee, Robert Kessy akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva aliyekuwa mgeni rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaviva, akihutubia.
Gwaride likiendelea.
Brass Band ya JKT ikiongoza Gwaride hilo.
No comments:
Post a Comment