Mama mjane akionyesha hati yake ya mirathi iliyotolewa na mahakama
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
(1977) inasema kila mtu ana haki ya kumiliki mali na haki ya hifadhi kwa mali
yake aliyonayo kwa mujibu wa sheria [Ibara 24(1)]. Haki hii inawahusu wanaume
na wanawake na chini ya Sheria ya Ardhi (1999) na Sheria ya Ardhi ya Vijiji
(1999), wanaume na wanawake wana haki sawa za kumiliki mali pia.
Mtu yeyote anaweza kuona kwamba sheria
hizi mbili pamoja na Katiba zinaweka wazi kuhusu haki ya kumiliki ardhi
Tanzania, lakini sivyo inavyotendeka katika sehemu mbali mbali za jamii yetu.
Matukio ya mjane kupoteza haki zake za mirathi baada ya kifo cha mume wake ni
tatizo sugu katika jamii nyingi hapa nchini.
Katika Mkoa wa Geita, Bi Msegena Jeremia
alifiwa na mume wake mwaka 2015 na kubaki na jukumu la kulea watoto sita peke
yake. Wakati akiwa bado na huzuni ya kuachwa na mume wake mpenzi, ndugu wa mume
wake waliitisha kikao kwa lengo la kugawana mali iliyoachwa na mume wake bila
ya kumshirikisha.
Kwa mujibu wa mila na desturi za kabila
la mume wake, mtoto mkubwa wa kiume ndiye anayemilikishwa mali iliyoachwa na
marehemu baba yake. Mume wa Msegena alikuwa na mtoto mkubwa kwa mke mwingine
anayeitwa Joshua. Huyu ndiye kikao cha wanandugu kilimfanya kuwa msimamizi wa
mirathi, ambayo ilikuwa ni nyumba, fedha zilizowekwa kwenye akaunti ya benki na
pikipiki.
Joshua alielekezwa ndugu wa baba yake
kutoa fedha zilizokuwa zimewekwa benki kwenye akaunti ya baba yake, ambazo
zilikuwa ni Sh1.9 milioni na kuziweka kwenye akaunti zilizofunguliwa kwa kila
mdogo wake ili kupata sehemu yao ya mirathi. Nyumba na pikipiki zilipangwa
kuuzwa.
Huu ulikuwa mwanzo tu wa mlolongo mzima
wa matatizo ya Msegena. Kwa mshangao mkubwa, Joshua aliweka fedha zote kwenye
akaunti yake binafsi na alivyoulizwa kwa nini alifanya hivyo kinyume na
utaratibu wa kisheria alimshambulia Msegena na kutishia kukata mikono yake.
Huku uhusiano kati ya Joshua na Msegena, ambaye ni mama yake wa kambo, ukididimia,
ndugu wa mume wake Msegena walishirikiana kumfukuza aondoke nyumbani.
“Joshua alinifungia nje ya nyumba na
nililala siku mbili kwa jirani bila ya kujali usalama wangu. Siku ya tatu
nilikosa uvumilivu, hivyo nilienda mjini kuomba msaada sehemu ambayo ningeweza
kuupata,” alisema Msegena huku machozi yakitiririka kwenye mashavu yake.
Kule mjini alibisha mlangoni kwa kila
aliyemfikiria angemsaidia akiamini atafunguliwa mlango ili atue mzigo wake
aliokuwa ameubeba kutoka kwa viongozi wa serikali za mitaa hadi polisi na
kwenye Mahakama ya Mwanzo. Moja ya matukio ya kugonga kwake kwenye mwamba ni
pale Joshua, ambaye sasa alikuwa na fedha nyingi aliweza kumhonga hakimu wa
mahakama ambaye aliamua kesi kwa upendeleo.
Hata hivyo, si kila ndugu wa mume wa Msegena
hakuguswa na changamoto alizokuwa akizipata baada ya kuachwa na mume wake
mpenzi. Wifi yake Msegena alikuwa anamfahamu msaidizi wa kisheria Geita, Bw
Bernard Mosira. Aliamua kumsaidia Msegena kwa kumtambulisha kwa msaidizi wa
kisheria ili apate msaada zaidi. Neema ilimjia Msegena kupitia Bernard Mosira,
ambaye aliamua kuwasiliana naye kwa lengo la kumsaidia.
“Nilimwita Bernard na kumwelezea tatizo
langu. Alinishauri nirudi nyumbani na aliahidi kwamba atawasiliana nami ili
anisaidie katika kesi hii,” alisema.
Baada ya kufika nyumbani, mwenyekiti wa
kijiji aliitisha mkutano ujulikanao kwa kimila kama “Nzengo” kwa lengo la
kumtenga na kumfukuza Msegena kijijini kwa madai kwamba alikuwa akijihusisha na
vitendo vibaya, ambavyo kwayo hastahili aishi kijijini pale.
Baada ya kusikia habari hizi za
kusikitisha, Bernard alisafiri hadi kijijini kwa Msegena siku iliyofuata na
kwenda kuwaona viongozi ili apate kumsaidia Msegena kutulia tena na kuishi kwa
amani huku akiendesha maisha yake na kuwaambia viongozi wa kijiji ambacho
kingewapata ikiwa wangeendelea na uamuzi wao wa kumtenga Msegena kwa lengo la
lengo la kumfanya akose haki zake za mirathi.
Hivyo, Bernard alitumia uzoefu wake
kumwelimisha Msegena juu ya sheria, haki na wajibu wake.
Akiwa na ujasiri baada ya kupata msaada
wa kisheria na yote yaliyotokea kwake kuhusiana na haki zake za miradhi
aliripoti yote aliyotendewa na Joshua jinsi alivyopelekwa kituo cha polisi na
kuwekwa ndani na kupelekwa Mahakama ya Mwanzo. Baada ya kusikiliza
ushahidi wote, Mahakama ilitoa uamuzi uliompa ushindi na ndugu wa mume wake
waliamriwa na Mahakama kutouza nyumba yake kama walivyokuwa wamepanga na
Mahakama ikasema Msegena ndiye mmiliki halali wa nyumba na pikipiki.
“Wakati wa kusikiliza kesi, niliongea
kama mtu anayejua sheria na watu walionisikia, hasa hakimu na polisi,
walishangaa huku wakijiuliza nilipata wapi elimu ya aina ile,” alisema Msegana.
“Tunafurahi kujifunza umuhimu wa kufuata
sheria na tumeenda mbele zaidi kwa kuwaalika Bernard na wenzake na wamekuja
hapa kijijini mara mbili kutusaidia kuelewa masuala ya kisheria wakati wa vikao
vyetu vya kawaida,” alisema mmoja wa viongozi wa kijiji.
Yaliyomkuta Msegena ni picha halisi ya
namna gani msaada wa kisheria unahitajika kwa watu, ambao haki zao za kisheria
zinavunjwa kwa kukosa msaada wa kisheria. Kwa msaada wa kisheria, pande mbili
za mgogoro zinaweza kupatana na kuafikiana tena. Ni jambo jema kuhamasisha
elimu kuhusu haki za wajane na pia kupiga vita mila na desturi kandamizi katika
jamii.
Kwa sasa Msegena ni mwanamke
anayejitambua na anaishi kwa uhuru huku akitambua haki zake za msingi kutokana
na msaada wa kisheria alioupata. Anaendesha maisha yake kwa kufuga kuku na
kulima mazao kwenye ardhi ambayo iko karibu na nyumba yake. Pikipiki, ambayo
hapo awali hakuwa na matumaini ya kuipata tena, anaitumia kubebea abiria na kwa
njia hiyo hujipatia fedha inayoongeza kipato chake na kumwezesha kutunza
familia yake.
No comments:
Post a Comment