Mkurugenzi wa Idara ya Hazina na Masoko ya Fedha wa Benki ya NBC,Peter Nalitolela akizungumza katika kongamano la siku moja kuhusu mitaji ya fedha na usimamizi wa hatari zinazoweza kutokea katika miamala ya kifedha kwa wadau kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Benki Kuu ya Tanzania, Tanesco, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kongamano hilo lilifanyika jijini Dodoma mwishoni mwa wiki.
BENKI ya Taifa ya Biashara (NBC), imesema itaendelea
kushirikiana kikamilifu na serikali ya awamu ya tano katika azma yake ya
kuwaletea wananchi wake uchumi wa kweli na maendeleo imeelezwa jijini Dodoma
mwisho mwa wiki.
Akizungumza wakati wa kongamano la wadau juu ya upatikaji
wa fedha na usimamizi wa hatari zinazoweza kujitokeza katika miamala ya
kifedha lililoandaliwa kwa wadau, Mkurugenzi wa Idara ya Hazina na Masoko wa
NBC, Peter Nalitolela alisema NBC imejizatiti kushirikiana na serikali na
taasisi zake katika kuhakikisha nchi inafaidika na kiasi cha pesa inachotumia
katika miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo inayoendelea
kufanyika.
Alisema kongamano hilo lililohudhuriwa na wadau kutoka Benki Kuu
ya Tanzania (BoT), Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tanesco, TPDC na
Wizara ya Fedha na Mipango lilikuwa na lengo kubwa ya kuangalia vyanzo
mbalimbali vya fedha vinavyopatikana katika miradi mbalimbali mikubwa
inayofanywa na serikali pamoja na kuangalia usimamizi wa hatari katika miamala
ya kifedha inayoweza kutokea katika miradi hiyo.
“Kama mjuavyo miradi mbalimbali mikubwa inayofanywa na serikali
ya awamu ya tano kama vile mradi wa reli ya kisasa (SGR), mradi wa umeme wa Mto
Rufiji wa Stiegler’s Gorge, ujenzi wa barabara na madaraja, baadhi ya miradi
hufanywa kwa mikopo kutoka pande tofauti, hivyo tulitaka kuonyesha uwezo wetu
kama NBC katika kusaidia upatikanaji wa fedha na pia linapokuja suala la
uzimamizi wa hatari za kifedha katika miamala hiyo.
“Kilicho kikubwa ni kwa NBC kuangalia uwezo wetu kwa njia
tofauti tofauti ikiwemo katika kukopesha, lakini pia kuona serikali haipati
hasara kutokana na masuala ya riba, fedha za kigeni na kushuka kwa thamani ya
shilingi, hivyo NBC tumejiandaa kushirikiana na serikali kikamilifu katika
kutimiza azma yake, kwa uwezo wetu tunaweza kushirikiana zaidi na zaidi”,
aliongeza Bwana Nalitolela.
Pamoja na hayo Mkurugenzi huyo alisema kama inavyofahamika kuwa
NBC inamilikiwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania, Benki ya Absa ya Afrika
Kusini pamoja na Benki ya Dunia,hii huiweka NBC katika nafasi nzuri ya kusaidia
juhudi za serikali.
Katika kongamano hilo pia NBC Ilileta wataalam kutoka benki mama
ya Absa ili kuweza kuonyesha uzoefu wao walioupata kupitia miamala waliyofanya
na serikali za nchi mbalimbali barani Afrika.
No comments:
Post a Comment