RC Hassani Khatibu atoa Neno kwa wenye Uwezo kusaidia Watoto Yatima - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Tuesday, May 12, 2020

RC Hassani Khatibu atoa Neno kwa wenye Uwezo kusaidia Watoto Yatima


Na Thabit Madai, Zanzibar.

MKUU wa Mkoa wa Mjini Magharib Unguja, Hassan Khatib Hassani amewataka watu wenye uwezo na taasisi za biashara kuwa na tabia ya kuwahudumia na kuwatunza watoto yatima ili jamii kuishi kwa usawa.

Wito huo ameutoa wakati akipokea msaada wa vyakula vya futari kwa ajili ya watoto yatima uliotolewa na Bank ya Afrika (BOA),Mazizini Mjini Unguja.

Mkuu wa Mkoa huyo alisema kwamba watoto yatima wanapaswa kuenziwa na kutunzwa kama watoto wengine hivyo jukumu hilo ni la kila mmoja.

Alisema kuwatunza watoto yatima kutapelekea watoto hao kuwaondolea unyonge na kupata jamii yenye maadili.

Pia alisema ili kuwa na jamii yenye maadili na kujali, ipo haja kwa kila mwenye uwezo kuwajali watu wasio na uwezo hasa mayatima kama inavyoelekezwa na vitabu vya dini.

“Msaada huu umekuwa na maana sana kwa kuwa mmewalenga mayatima kwani kufanya hivyo sehemu ya utekelezaji wa ibada kama alivyotuhimiza Mwenyezi Mungu kuwa tulisaidia kundi hili,” alieleza Hassan.

Aidha aliwataka wazazi na walezi kuzingatia wajibu wao kwa kuwalea watoto hao katika maadili mema sambamba na kuwalinda dhidi ya majanga yakiwemo maradhi ya covid 19 yanayosababishwa na virusi vya corona.

Alisema iwapo wazazi watashirikiana na kuwadhibiti watoto wao, kuna uwezekano kuwaepusha na maambukizi ya maradhi hayo yaliyoenea ulimwenguni.

“Iwapo wazazi hasa kina mama mkitukazania kina baba na watoto kujilinda dhidi ya corona, sote tunaweza kuwa salama,” alisema RC Hassan.

Akizungumza kabla ya kukabidhi msaada huo, Meneja wa Banki ya  Afrika (BOA) tawi la Zanzibar, Juma Burhan Mohamed alieleza kuwa msaada huo ni sehemu ya utaratibu wa benki hiyo kutumikia jamii.

Alisema benki hiyo imekuwa na utaratibu wa kutoa misaada mbali mbali kwa jamii ikiwemo ya futari katika mwezi wa ramadhani, hivyo kwa mwaka huu iliamua kutoa kwa kundi hilo baada ya kuzingatia hali halisi ya maradhi.

“Kikawaida kila mwaka huwa tunafutari pamoja na wateja wetu sambamba na kutoa misaada kwa watu wenye mahitaji ila kutokana na maradhi tumeamua kutoa vyakula vikavu kwa watoto yatima ili nao waweze kufunga kwa urahisi zaidi,” alisema Mohamed.

Akizungumza kwa niaba ya wazazi na walezi wengine, Mama Mlezi Mkuu wa kituo cha kulelea watoto yatima Mazizini pili saadalla mussa alieleza kuwa msaada huo umetolewa kwa watkati muafaka na kuahidi kuwa utatumika kama ulivyokusudiwa.

“Kwa niaba ya Idara ya Ustawi wa Jamii na wizara kwa ujumla tunaishukuru benki ya BOA kwa kutusaidia kwani licha ya kupata huduma kutoka serikalini, bado tuna mahitaji ambayo yanapaswa kutoka kwa watu binafsi kwani watoto hawa ni wa jamii nzima,” alieleza mama huyo.

Msaada huo ambao uliogawiwa kwa familia zinazolea watoto yatima wa mkoa wa Mjini Magharibi, BOA ilikabidhi mchele, sukari, unga wa ngano na mafuta ya kupikia katika hafla iliyofanyika katika ofisi za baraza la manispaa Magharibi ‘B’ na kituo cha kulelea watoto yatima Mazizini.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages