STRAIKA wa kimataifa wa Zambia, Justin Shonga, amekubali kujiunga na Simba huku akitoa masharti kwa uongozi wa timu hiyo kwa kuwataka kuongea na mabosi zake wa Orlando Pirates.
Mzambia huyo amekuwa akihusishwa kutakiwa na Simba tangu msimu uliopita wakati ilipokuwa nchini ya Mbelgiji, Patrick Aussems kabla ya kufungashiwa virago na mikoba yake kuchukua Mbelgiji mwenzake, Sven Vandenbroeck ambaye ni kocha wa zamani wa timu ya taifa ya Zambia ‘Chipochipolo’.
Kwa mujibu wa jarida la Kickoff kutoka nchini Afrika Kusini, Mzambia huyo ni miongoni mwa wachezaji kumi wenye thamani kubwa katika Ligi Kuu ya Afrika Kusini, akiwa na thamani ya euro 600,000 sawa Sh bilioni 1.5 za Kitanzania.
Simba imekuwa ikihaha kusaka saini ya nyota huyo ambaye amekuwa hana msimu mzuri katika timu yake ya Orlando Pirates kufuatia msimu huu kucheza mechi nane pekee bila ya kufunga bao lolote tofauti na misimu miwili iliyopita ambapo alifanikiwa kucheza jumla ya mechi 48 huku akifunga mabao 12 na akitoa asisti kumi.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka Zambia, moja kati ya vitu wanavyotamani Wazambia ni kuona nyota huyo anarudi kwenye ubora wake ikiwezakana nje ya timu hiyo.
“Shonga ni mchezaji mzuri na amekuwa akihusishwa na klabu nyingi, siyo Simba peke yake na upande wa mashabiki wa hapa Zambia wamekuwa wakitamani kumuona akirejea kwenye ubora wake, ingawa yeye ndiye mhusika wa mwisho wa kujua wapi anatakiwa kwenda,” alisema Methiew Kambamba, mmoja kati wachambuzi wa soka kutoka Zambia.Championi lilifanikiwa kumpata mshambuliaji huyo ambaye alisema:
“Sijapata hizo taarifa, ndiyo nasikia kwako lakini kama ni kweli nitakuwa tayari ikiwa wao watafuata utaratibu wa kuongea na waajiri wangu halafu mambo mengine yakafuata.” Ikumbukwe kuwa msemaji wa timu hiyo, Thandi Merafe alinukuliwa na Gazeti la Sporti Xtra akisema kwa upande wao wapo tayari kumuachia nyota huyo ikiwa watapokea ofa ya maana kutoka kwa timu yoyote. Kama dili la kumsajili Shonga likifanikiwa, Simba itakuwa imetimiza ule msemo wake wa timu ya Next Level kwa kuwa Mzambia huyu ni mmoja wa wachezaji wa kariba ya timu kubwa za Afrika.
No comments:
Post a Comment