Kanisa la Anglikana Tanzania limetuma salamu za pole kwa Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kufuatia kifo cha Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mh Benjamini William Mkapa aliyefariki dunia usiku wa Julai 24-2020.
Akitoa salamu hizo Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania Dkt Mahimbo Mndolwa amesema Kanisa linatambua mchango mkubwa wa Mzee Mkapa katika kusaidia maendeleo ya huduma za Kanisa kabla ya kuwa Rais, akiwa Rais na hata baada ya kustaafu kwake.
“Kipekee ninaenzi huduma yake ya kuwezesha Kanisa Anglikana Tanzania kuwa na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Yohana (St John’s University of Tanzania) cha Jijini Dodoma”
Mzee Mkapa alipenda watu wake, alipenda kanisa na daima alikuwa ni muumini wa kielelezo kwa wengi” alisema Dkt Mahimbo.
Aidha Dkt Mahimbo alimuelezea Mzee Mkapa kama mtu jasiri aliyekuwa mstari wa mbele katika kusaidia masuala mbalimbali yanayohusu Madhehebu na imani za watanzania.
“Tunakumbuka wakati mwingi tulipomwomba katika matukio mbalimbali hakusita kufika na alitusaidia” aliongea Dkt Mahimbo.
Amesema kuwa kwa kutazama mambo makubwa aliyoyafanya kwenye Maisha yake kuna kila sababu ya kumtukuza sana Mungu na kwamba kama kanisa wanaiombea familia yake na watanzania wote ili Mungu akizidi kuwa faraja katika kipindi chote cha msiba.
No comments:
Post a Comment