YANGA yamfukuza KOCHA wake! - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, July 27, 2020

YANGA yamfukuza KOCHA wake!


Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

Klabu ya Yanga imetangaza kuachana na aliyekuwa kocha wao Luc Eymael kutoka na kutoa kauli za kibaguzi kwa mashabiki wa soka nchini baada ya mchezo wa mwisho wa ligi kuu bara dhidi ya lipuli FC jana.

KOCHA Mbelgiji, Luc Eymael amefukuzwa kazi Yanga SC baada ya miezi saba tu kazini kutokana na kutoa kauli zilizotafsiriwa kama za kibaguzi dhidi ya mashabiki.

Taarifa ya Yanga kwa vyombo vya Habari leo imesema kwamba kutokana na kauli hizo za kibaguzi uongozi umeamua kumfuta kazi Eymael kuanzia leo (Julai 27, 2020) na kuhakikisha anaondoka nchini haraka iwezekanavyo.

“Uongozi wa klabu ya Yanga umesikitishwa na kauli zisizo za kiungwana na za kibaguzi zilizotolewa na Kocha wake Luc Eymael na kusambaa katika mitandao ya kijamii,” imesema taarifa ya Yanga na kuongeza;

“Baadhi ya kauli hizo za Kocha Luc Eymael amesikika akitoa kauli za kuwashutumu Mashabiki kwamba hawana elimu, watu kwenye nchi hii ni wapumbavu, mashabiki hawajui mpira kazi yao ni kupiga kelele kama nyani na mbwa, Viongozi wa Klabu ni sifuri na shirikisho la mpira wa miguu Tanzania lipo kwa ajili ya Simba tu,”.



Aidha, Uongozi wa Yanga umewaomba radhi viongozi wa nchi, Uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Viongozi wa Klabu ya Simba, wanachama, wapenzi na mashabiki wa Yanga, pamoja na wananchi kwa ujumla kutokana na kauli za kuudhi na kudhalilisha zilizotolewa na kocha huyo.

“Klabu ya Yanga inathamini na kuamini katika misingi ya nidhamu na utu, na inapingana na aina yoyote ya Ubaguzi,”imeongeza taarifa hiyo iliyosainiwa na kaimu Katibu Mkuu wa klabu, Wakili Simon Patrick.

Eymael anaondoka Yanga SC baada ya kuiongoza timu katika mechi 32 tangu ajiunge nayo Januari ikishinda 16, sare 11 na kufungwa tano.

Anaondolewa siku moja baada ya kuisaidia Yanga SC kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kufuatia ushindi wa 1-0 dhidi ya wenyeji, Lipuli FC jana Uwanja wa Samora mjini Iringa, bao pekee, David Molinga Ndama ‘Falcao’ dakika ya 38.

Kwa ushindi huo, Yanga SC imefikisha pointi 72 na kumaliza ikizidiwa pointi 16 na mabingwa, Simba SC na wakiwazidi pointi mbili Azam FC waliomaliza nafasi ya tatu.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages