Kuelekea mfungo wa Ramadhan, Mkurugenzi wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela leo ameambatana na familia yake pamoja na wafanyakazi wa benki hiyo kotoa sadaka ya futari ya thamani ya shilingi milioni 10 kwa vituo 5 vya watoto yatima katika mkoa wa Dar es Salaam.
Hafla hiyo ilifanyika katika viwanja vya Karimjee na kutanguliwa na ibada ya Ijumaa iliyoongozwa na Imam, Haroub Khamis katika Masjid ya Karimjee. Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Nsekela amesema sadaka hiyo ni sehemu ya shukrani ya familia yake na muendelezo wa utamaduni wa Benki ya CRDB kutoa sadaka kwa makundi yasiyojiweza na kuandaa futari maalum kwa ajili ya wateja na wadau wake katika mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhan.
“Tukikaribia kuanza Mwezi Mtukufu wa Ramadhan ambapo mioyo na fikra vipo katika kumnyenyekea Muumba tumeona ni jambo la faraja kujumuika kwa pamoja na watoto yatima katika ibada hii ya funga kwa kuwapatia msaada wa futari,” alisema Nsekela huku msaada huo pia utatolewa katika vituo vya watoto yatima katika kanda zote nchini.
Akisisitiza juu ya umuhimu wakuwasaidia watu wasiojiweza, Nsekela alisema katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni vyema jamii ikafahamu wapo watu ambao iliwaweze kutimiza funga yao kikamilifu wanahitaji msaada kutoka kwa wale ambao wenye uwezo.
“Kutoa msaada kwa watu wasiojiweza ni kujitafutia thawabu, lakini pia kunasaidia kudumisha upendo kwa ndugu, jamaa, marafiki na jamii kwa ujumla wake. Hata katika Quran takatifu Surah Al-Baqarah aya ya 2:83, Mwenyezi Mungu ametuamrisha kuwasaidia yatima na wasiojiweza,” aliongozea Nsekela.
Akipokea msaada huo kwa niaba ya vituo vya watoto yatima, Sheikh Issa Othman Issa amemshukuru Nsekela na familia yake pamoja na wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa msaada huo huku akitanabaisha kuwa kusaidia wasiojiweza wakati wa mfungo wa Ramadhan ni ibada na kunafungua milango ya baraka.
“Mafundisho ya Mtume SAW yanatuambia atakayemfuturisha aliye na swaum atapata thawabu kama zake bila ya mwenye swaum kupungukiwa na kitu. Kwa niaba ya vituo hivi na watoto hawa niwashukuru sana na Mwenyezi Mungu aendelee kuibariki Benki yetu ya CRDB,” alimalizia Sheikh Issa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kituo cha Amani Foundation for Orphans, Hajjaty-Zubeida Abdallah kilichopo Wilaya ya Kigamboni, aliishukuru kwa msaada huo akisema umekuwa faraja kwa watoto hao na utawasaidia kukamilisha funga yao ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhan kikamilifu.
“Mkurugenzi Mtendaji kwa niaba ya vituo hivi nikushukuru sana kwa msaada huu, nichukue pia fursa hii kuwakaribisha katika vituo vyetu ilituweze kujadiliana kwa pamoja namna bora ya kuwasaidia watoto wetu hawa,” alisema Hajjaty-Zubeida.
Vituo vilivyopatiwa msaada huo ni pamoja na Kituo cha Tarbia kilichopo Wilaya ya KinondonI, Kituo cha Irshad Islamic kilichopo Wilaya ya Ubungo, Kituo cha Amani Foundation for Orphans kilichopo Wilaya ya Kigamboni, Kituo cha Hiyari Orphans kilichopo Temeke, Kituo cha Busara Orphans kilichopo Wilaya ya Ilala.
Kila kituo kimepatiwa Unga wa Ngano kilo 50, Sukari kilo 50, Maharage kilo 50, Tambi pakiti 30, Tende pakiti 20, Mafuta lita 20, Njugu kilo 20, Sabuni za Unga za Kufulia Ndoo 5 pamoja na maziwa ya unga makopo makubwa 5 sambamba na majani ya chai pakiti 10.
No comments:
Post a Comment