TIRA YAWANOA WANAHABARI, MAWAKILI HUDUMA ZA BIMA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Sunday, June 23, 2024

TIRA YAWANOA WANAHABARI, MAWAKILI HUDUMA ZA BIMA

Meneja wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) Kanda ya Ziwa, Richard Toyota, leo jijini Mwanza, akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo mawakili na waandishi wa habari (hawapo pichani), kuhusu huduma za bima.
Baadhi wa waandishi wa habari wakifatilia mada katika mafunzo ya kuwajengea uwezo kuhusu huduma za bima yaliyoshirikisha pia mawakili. Kushoto ni Meneja wa NIC Kanda ya Ziwa, Stella Marwa.
Mwanasheria Mwandamizi wa TIRA Kanda ya Ziwa, Wakili Aderickson Njunwa, leo akifafanua kwa waandishi wa habari na mawakili (hawapo pichani), shughuli mbalimbali za bima ikiwemo fidia, madai, malalamiko na migogoro ya bima.
Waandishi wa habari na mawakili wakifuatilia mada mbalimbali za huduma za bima katika mafunzo ya kuwajengea uwezo yaliyofanyika leo jijini Mwanza.
Wana habari na mawakili wakimsikiza Mwanasheria wa Mwandamizi wa TIRA Kanda ya Ziwa, Wakili Aderickson Njunwa.
Viongozi wa TIRA, NIC na MPC wakiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari na mawakili leo baada ya mafunzo.

Na: Baltazar Mashaka, Mwanza

MAMLAKA ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Kanda ya Ziwa imesema licha ya Watanzania milioni 40 kutegemea kilimo na kuchangia pato la taifa kwa asilimia 6.7 wanakabiliwa na changamoto ya kutokata bima ya kukinga mazao yao dhidi ya athari za ukame, magonjwa na majanga.

Pia sekta hiyo ya kimkakati serikali imetengea fedha kwa ajili ya skimu ya umwagiliaji ili kuwawezesha wakulima walime kwa tija watoke katika kilimo cha kujikimu kwenda kilimo biashara chenye tija kikiambatana na bima.

Hayo yameelezwa leo na Meneja wa TIRA, Kanda ya Ziwa, Richard Toyota wakati akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari na mawakili jijini Mwanza, wafahamu huduma za bima, ukiwa ni mwendelezo wa mamlaka hiyo kutoa mafunzo na elimu ya umuhimu wa huduma hizo kwa wadau mbalimbali.

Amesema kilimo ni uti wa mgongo ni eneo la kimkakati linalotegemewa na wakulima milioni 40 sawa na asilimia 65.6 ya Watanzania, hivyo mafunzo hayo yatawasaidia waandishi wa habari na mawakili kufahamu masuala ya bima na hivyo kuelimisha wananchi wakiwemo wafugaji na wakulima umuhimu wa kukata bima ya mazao na mifugo.

Toyota amesema serikali imewekeza katika mifumo ya bima kwa ajili ya utoaji taarifa za bima, hivyo ni muhimu wananchi wakafuatilia na kuzingatia taarifa hizo ili kuondokana na changamoto wakati wa majanga.

Naamini kupitia kalamu zenu mtafikisha elimu sahihi kwa umma, itakayosaidia jamii kufahamu ni namna gani shughuli zao zinaweza kufungamanishwa na bima zikawa na tija katika mnyororo wa kilimo ambao unachangia asilimia 6.7 katika pato la taifa na hivyo mchakato wa bima utaboresha sekta ya kilimo na huduma za bima,” amesema.

Meneja huyo wa TIRA Kanda ya Ziwa amesema waandishi wa habari baada ya kupata elimu watakuwa mabalozi wazuri na walaji wa bima, watasaidia Watanzania wasiofahamu taratibu za kudai haki zao, watataumia sekta ya bima kuwekeza mitaji yao ili kuondokana na utegemezi.

Amesema huduma za bima zimeongezeka ikiwemo afya, vyombo vya moto, nyumba na kilimo, hivyo ni vyema wananchi wakajiunga na huduma hizo ili kupata fidia wakati wa majanga, mfano kwenye magari wahakikishe wanapewa tiketi ambayo ni uthibitisho wa kupata haki na wasikubali kupanda yasiyo na bima kuepuka changamoto ya fidia ikitokea ajali.

Mwanasheria Mwandamizi wa TIRA Kanda ya Ziwa, Wakili Aderickson Njunwa, amesema waandishi wa habari na mawakili wanayo nafasi kubwa ya kuelimisha wananchi kuhusu huduma za bima ili kupata haki za madai, malalamiko na migogoro inayohusu bima.

Waandishi wa Habari tunaamini mkipata taarifa sahihi mtaifikia jamii kwa urahisi na elimu hiyo ya bima itakuwa sahihi, kwa kutambua hilo ndiyo maana tumekutana ili tukae pamoja, tupeane elimu ili mfahamu TIRA inafanya nini katika jamii,” amesema.

Kwa upande wake Meneja wa Shirika la Bima la Taifa (NIC), Kanda ya Ziwa, Stella Marwa amesema kuna aina tatu za bima ya kilimo (bima mseto, hali ya hewa na maeneo maalum), zinakatwa ili kuwakinga wakulima na wafugaji wanufaike na mazao yao pamoja na mifugo yao.

Naye Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza (MPC), Edwin Soko amesema; "Tuwe mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu bima ambapo MPC kwa kushirikiana na TIRA tunaweza kuanzisha tuzo za waandishi bora za bima ili kuhamasisha zaidi uandishi wa habari hizo.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages