Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar imepongeza uzalendo na kujitoa kwa watendaji wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kuendeleza na kukamilisha miradi mbalimbali inayotekelezwa na Shirika hilo kwa mafanikio makubwa.
Hayo yameelezwa na Kiongozi wa Timu ya Wataalamu kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar wanaoandaa Sera ya Uendeshaji wa Mashirika ya Umma, Saleh Said Mubarak, wakati wa ziara yao ya kutembelea miradi ya NHC iliyofanyika leo, Desemba 18, 2024, jijini Dar es Salaam.
Mubarak alisema kuwa katika ziara hiyo wamejionea uwajibikaji mkubwa wa menejimenti na watumishi wa Shirika hilo, hali iliyowezesha kusimamia miradi wanayotekeleza kwa mafanikio makubwa.
“Leo tumetembelea miradi mikubwa ya NHC kujifunza namna bora ya kusimamia miradi mbalimbali ya Serikali. Hii imetupa mwamko mpana wa kutambua njia za kupita katika kusimamia miradi inayotekelezwa na taasisi za Serikali,” alisema Mubarak.
Aidha, Mubarak alibainisha changamoto kubwa kwa baadhi ya watendaji wa taasisi za Serikali kukosa weledi na kufanya kazi kwa mazoea, hali inayosababisha kuzorotesha kasi ya maendeleo na ukamilishaji wa miradi. Alipongeza NHC kwa uwajibikaji mkubwa wa wasimamizi na wafanyakazi wote wanaoshiriki katika miradi hiyo.
Kwa upande wake, Afisa Habari Mkuu wa NHC, Yahya Charahani, alisema kuwa mafanikio ya utekelezaji wa miradi hiyo yanatokana na dhamira ya dhati ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alitoa fedha za kuendeleza miradi iliyokuwa imesimama kwa muda mrefu.
“Sisi kama Shirika la Nyumba la Taifa tunaishukuru sana Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wetu, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuiokoa miradi hii. Sasa miradi inakwenda vizuri, na mradi wa Morocco Square umekamilika kabisa. Kweli wananchi wameifurahia na wanapata fursa mbalimbali kupitia miradi hii,” alisema Charahani.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na:Mradi wa 711 Kawe: Lengo lake ni kutoa makazi bora kwa wananchi kupitia majengo ya kisasa yenye miundombinu muhimu.
Samia Housing Scheme: Mradi unaolenga kuboresha makazi kwa wananchi wa kipato cha kati na cha chini, ambao unatekelezwa kwa kasi kubwa.
Morocco Square: Mradi huu uliokamilika umefanikiwa kutoa fursa za biashara na huduma za kijamii, na umekuwa kivutio kikubwa kwa wananchi.
Mubarak alisisitiza kuwa Samia Housing Scheme ni mradi wa kihistoria wenye lengo la kujenga nyumba 5,000 kwa awamu, hatua ambayo itasaidia kupunguza changamoto ya makazi nchini.
“Kwetu sisi, hili ni somo zuri la kuona jinsi tunavyoweza kusaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ili iweze kutoa huduma bora za makazi kwa wananchi wake. NHC mmeliweza kwa kiwango kikubwa kwani mnaendelea kuhakikisha wananchi wanapata makazi bora,” alisema Mubarak.
Kwa kumalizia, timu ya wataalamu hao walielezea kuridhishwa kwao na juhudi za Serikali ya Tanzania kuhakikisha miradi ya NHC inakamilika kwa mafanikio makubwa. Walisema kuwa miradi hiyo itakapokamilika, itaongeza mapato ya Shirika na Serikali, na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
No comments:
Post a Comment