Upatu: Mbinu yakujikwamua yenye tamu na chungu - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, January 27, 2025

Upatu: Mbinu yakujikwamua yenye tamu na chungu

KUCHEZA upatu imekuwa ni mtindo ambao wanawake wengi wamekuwa wakiutumia kama njia ya kujikwamua kupata fedha au mtaji kwaajili ya kuendesha shughuli mbalimbali za maisha yao ya kila siku.

Wanawake saba katika kundi la wanawake 10 waliofanya mahojiano na makala haya wamewahi kushiriki katika aina mbalimbali za upatu.

Hata hivyo mtindo huo umekua ni fursa yenye tamu na chungu inayowakabili wanawake wengi kutokana na changamoto za mfumo wa uendeshaji wake.

Upatu upo aina mbalimbali kulingana na mfumo wa uendeshaji wake, kwa mfano upatu wa hisa ambao kundi la wanawake wanaungana katika kuweka kiasi kidogo kupata fursa ya kukopa kiwango maalumu bila riba ya marejesho.

Pia kuna aina ya upatu unaohusisha vikundi vya ushirika, upatu wa vikundi vidogo vya uwekaji na ukopaji kwa riba ambao maarufu mitaani kama (kausha damu), na nyengine.

Upatu unafanyika katika maeneo ya kazi mfano maofisini, majirani, na hata kwa wanafamilia.

Mtindo uliozoelekea zaidi upatu ni wa vikundi vidogo vya wasichana na wanawake katika maeneo ya makazi ambao wanaungana na kuweka utaratibu wa kuchangiana kiwango maalumu cha pesa ambacho kila mshiriki atalazimika kutachangia kila baada ya muda.

Vikundi hivi ambavyo mara nyingi inakuwa ni majirani, marafiki au familia vinakuwa na kiongozi maalumu anaechaguliwa miongoni mwa wanakikundi maarufu kama “kijumbe”.

Kazi ya kijumbe ni kukusanya michango ya washiriki, kutunza fedha za kikundi, na kusimamia ugawaji wa fungu kwa washiriki kulingana na zamu za upokeaji na idadi ya washiriki.

Halima Hassan mmoja wa washiriki wa upatu kutoka Manzese Dar es Salaam ameeleza kuwa kikundi chao cha upatu kilikuwa na wanawake 10 katika mtaa wao, ambao walikubaliana kila mmoja atachangia shilingi 5,000 kila ijumaa ya wiki na kukabidhiwa kijumbe.

Vilevile walikubaliana kila ijumaa “anatoka mtu mmoja”, akimaanisha kila siku ya ijumaa ya wiki mshiriki mmoja katika zamu ya kupokea anapewa shilingi elfu hamsini hadi mzunguko wa watu 10 utakapotimia.

Kupitia upatu imekuwa fursa nzuri kwa wakina mama wengi kama mbinu ya kujikwamua na kupata kipato kumudu gharama za maisha ya kila siku na familia zao, au mtaji wa kujiendeleza katika biashara ndogondogo.

Saida Hamad kutoka Unguja Zanzibar ameeleza yeye kupitia upatu aliowahi kucheza kazini kwake aliweza kupata shilingi laki 5 ambazo alizitumia kama mtaji wa kuanzisha duka la kuuza vyakula la rejareja maarufu, ameeleza mradi huo unamuezesha kuongeza njia ya ziada ya kuzalisha kipato mbali na kazi yake anayofanya sasa na inamsaidia kumudu majukumu mbalimbali ya familia yake.

Mshiriki mwengine Irene Malisa mkazi wa Kimara Dar es Salaam ameeleza makala haya kuwa kupitia upatu yeye ameweza kupata ada ya kulipia skuli kwa kijana wake.

Alisema bila ya hivyo angepata wakati mgumu ukizingatia kipindi cha mwezi Januari ulivyokuwa na hali ngumu kifedha. Irene ameongezea kuwa yeye pia anatumia upatu kama njia ya kupata mtaji rahisi usio na riba ya marejesho na masharti magumu ukilinganisha na mikopo ya kibenki.

Hata hivyo, mtindo huu wa upatu unakabiliwa na changamoto nyingi zinazotoka na kama mfumo wa uendeshaji wake, kukosa uaminifu kwa baadhi ya washiriki, kukosa elimu sahihi ya matumizi ya fedha na mengine, mambo haya yanageuza fursa hiyo tamu kuwa chungu.

Kwa mfano, wengi katika wanawake wanatumia pesa za upatu kujikimu kimaisha au katika matumizi ya kawaida kama kulipia michango ya harusi, kununua nguo, kununua chakula au kufanya starehe. Jambo hili linapelekea licha ya wengi kushiriki upatu kwa muda mrefu wameshindwa kupiga hatua za maendeleo kimaisha.

Changamoto nyengine ni ya kukosa uaminifu miongoni mwa wanakikundi, mfano inatokea mshiriki kujitoa baada ya zamu yake ya kupokea fungu inapopita au kugoma kuchangia wengine.

Au kwa namna nyengine mshika fedha ambaye ni “kijumbe” anaweza kutoweka na fedha za kikundi kwa kudai kuibiwa au kwa kuzitumia katika mambo binafsi na kushindwa kuzirejesha.

Saida Shamis kutoka Pongwe Tanga ameeleza yeye amewahi kushiriki upatu ambao kijumbe alitumia michango ya kikundi kugharamia matibabu ya mwanawe, ingawa aliahidi kurejesha lakini mpaka mwisho hakufanya hivyo.

Matokeo ya changamoto yamekuwa si mazuri kwa baadhi ya wanawake wanaoshiriki upatu, wengine wanalazimika kupoteza vyombo vyao vya ndani kama samani, vifaa vya eletroniki mfano televisheni au jokofu ili kufidia madeni wanayodaiwa.

Vilevile, upatu umezusha migogoro ya kijamii baina ya majirani au familia na hata kwa wanandoa, ushiriki wa harakati za upatu unafanya wanawake wengine kukosa utulivu majumbani na baadhi wanashawishika kujingiza katika vitendo viovu kama njia ya kujipatia kipato ili kupata fedha ya kuchangia katika kikundi.

Taasisi za kifedha kama mabenki wanaweza kutoa elimu ya fedha kwa vikundi mbambali vyaupatu kwa wanawake, mafunzo yanaweza kutolewa kuhusiana na namna nzuri kuendesha vikundi, urasimishaji wa vikundi, na kubuni utaratibu mzuri wa usajili wa washiriki katika kikundi ili kuepuka changamoto ya kujiengua bila utaratibu.

Pia mafunzo yanaweza kutolewa kuhusiana matumizi sahihi ya fedha, namna ya kuanzisha biashara ndogondogo, hii itawezesha wanawake wengi kutumia kipato kupitia upatu kujiendeleza kuliko katika matumizi ya kawaida.

Pia, vikundi vinaweza kupewa elimu kuhusu namna nzuri ya kuhifadhi amana na michango yao kwa kufungua akaunti za benki, jambo hili litawezesha kuhakikisha usalama wa fedha za zakikundi na kuzuia mianya ya upotevu na matumizi yasiyo rasmi.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages