Rais Mstaafu na Kamishna
wa Kamisheni ya Kupendekeza Namna Bora ya Kugharamia Fursa ya
Elimu Duniani (Education Commission on Financing Global
Education Opportunity) juzi tarehe 21 Machi, 2017, amekutana na Rais wa
Jamhuri ya Congo alipomtembelea Ikulu yake jijini Brazaville.
Katika nafasi yake ya
Mjumbe Maalum wa Kamisheni hiyo, Rais Mstaafu amemkabidhi Rais Sassou
Nguesso Ripoti ya Kamisheni hiyo yenye mapendekezo ya namna Dunia inavyoweza
kukabili janga la Elimu kwa kuwekeza katika Mpango wa Kizazi
cha Elimu (A Learning Generation). Mpango huo unalenga kuleta mapinduzi
makubwa ya Elimu katika nchi zinazoendelea ndani ya Kizazi Kimoja (miaka
30). Azma kuu ya Mpango huo ni kuwezesha ifikapo mwaka 2040, watoto wote kote
duniani wawe wanapata elimu iliyo sawa, na kwa kiwango cha ubora unaolingana
dunia nzima.
Kwa mujibu wa ripoti
hiyo, kwa sasa, hali ya elimu katika nchi zinazoendelea inalingana na ile
ambayo nchi zinazoendelea zilikuwapo miaka 70 iliyopita. Aidha, ripoti
inasisitiza kuwa, ikiwa nchi zinazoendelea zitaendelea kwa kasi ya sasa,
itazichukua nchi hizo kati ya miaka 90 na 110 kufikia viwango vya sasa vya nchi
zilizoendelea. Aidha, ripoti inatahadharisha kuwa takribani ajira bilioni 2
zitakufa ifikapo mwaka 2050 kutokana na maendeleo ya teknolojia, ambapo
asilimia 70 ya kazi hizo ziko katika nchi zinazoendelea. Hivyo, nchi
zinazoendelea zinapaswa kuangalia upya aina ya elimu na stadi zinazotolewa ili kuendana
na wakati ujao.
Kwa ajili hiyo, Kamisheni
inapendekeza njia mpya na bora za kufanya mageuzi katika elimu ikiwemo kuongeza
usimamizi, kupanua fursa, kuingiza ubinifu na teknolojia na kuongeza uwekezaji
katika elimu kwa kushawishi ushiriki wa Jumuiya ya Kimataifa na Sekta Binafsi.
Iwapo mapendekezo hayo yatatekelezwa, nchi zinazoendelea zinaweza kufidia pengo
hilo ndani ya miaka 30 ijayo. Rais Mstaafu ameiomba Namibia kujiunga na
Mpango huo.
Rais Mstaafu amempongeza
Rais Nguesso kwa mafanikio makubwa ambayo Congo imeyapata katika sekta ya
elimu ikiwemo hususan elimu ya awali na msingi. Kwa mujibu ya Ripoti ya
Kamisheni, endapo itafanya mageuzi yanayopendekezwa, Congo ina
uwezekano mkubwa wa kufanikiwa kuwa na Kizazi cha Elimu ifikapo mwaka 2040.
Kwa upande wake,
Rais Nguesso amepokea kwa furaha taarifa hiyo na kuelezea nia na
dhamira ya nchi yake ya kujiunga na Mpango wa Kizazi cha Elimu.
Ameelezea utayari wa nchi yake kufanya mageuzi katika sekta ya
elimu na kushirikiana na Kamisheni katika kufaniklisha azma hiyo. Amesisitiza
umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kuongeza fedha na uwekezaji katika sekta
ya elimu katika nchi za kati na zinazoendelea.
Rais Mstaafu amemaliza
ziara yake nchini Congo na kuelekea nchini Ghana kukutana na Rais wa Ghana Mhe.
Nana Akufo-Addo.
No comments:
Post a Comment