Baada ya Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kumfungia mechi mbili beki wa Simba, Abdi Banda ambapo tayari adhabu hiyo ameshaitumikia, beki huyo amesema hatarudia tena kosa hilo.
Aprili 2, mwaka huu, Banda aliingia matatizoni kwa kumpiga ngumi nahodha na beki wa Kagera Sugar, George Kavila kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba wakati timu hizo zikipambana.
Banda alipelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu kwa kosa
hilo la kumpiga Kavila na kuadhibiwa kwa adhabu ambayo alishaitumikia kwani
alisimamishwa kucheza mechi yoyote hadi suala lake litakaposhughulikiwa.
Akizungumza Banda alisema: “Namshukuru Mungu suala
langu limeisha, nimekoma na kuna kitu nimejifunza maana nilijiona mkosefu kwa
kujadiliwa na watu wengi.
“Sitarudia tena kitendo kama kile licha ya mchezo wa
soka kuwa na majaribu mengi ambayo yanaweza kukufanya uchukue uamuzi wowote
ule, nimejifunza na kuanzia sasa mimi ni mtu mwema.
“Kusimamishwa mechi mbili hakukuniathiri kwa
kuwa mimi ni mchezaji mkubwa ila ninachokiangalia hivi sasa ni kuisaidia timu
yangu iweze kutwaa ubingwa.”
Hata hivyo, kanuni za ligi kuu zinaweka wazi kwamba
mchezaji anayepigana au kupiga uwanjani anafungiwa kucheza mechi tatu au zaidi,
habari kutoka kwenye kamati hiyo zinasema Banda aliomba msamaha.
“Pia tumeona Banda ni mtu muhimu katika kikosi cha
Taifa Stars ambacho kina mechi hivi karibuni ndiyo maana ikawa hivi,” alisema
mmoja wa maofisa wa TFF.
No comments:
Post a Comment