WAZIRI wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe amesema yuko tayari
kuuachia uwaziri ili aweze kulithibitishia Bunge kuwa aliyekuwa waziri mkuu,
Edward Lowassa alihusika katika kashfa ya Richmond.
Dk. Mwakyembe
alitoa kauli hiyo jana bungeni baada ya Mbunge wa Arumeru Mashariki (Chadema),
Joshua Nassari na Mbunge wa Ubunge Ubungo (Chadema) Said Kubenea kumtuhumu juzi
kuwa hakutenda haki mwaka 2008 wakati alipoongoza Kamati Teule ya Bunge
kuchunguza kampuni tata ya ufuaji umeme ya Richmond bila kumhoji Lowassa ambaye
alituhumiwa.
Nassari juzi
wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais- Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi) alisema Dk. Mwakyembe ameikataa ripoti iliyomchunguza Mkuu wa Mkoa
wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha televisheni cha Clouds kwa madai kuwa
haikumhoji mkuu huyo wa mkoa ili hali yeye aliendesha Kamati ya Teule ya Bunge
ya Richimond na kumuondoa madarakani Lowassa, licha ya kutokumhoji.
Akijibu tuhuma
hizo, Dk. Mwakyembe alisema ni kazi ngumu kwa sasa kumsafisha Lowassa kuhusu
tuhuma zilizokuwa zinamkabili kuhusu Richmond.“Naomba nimalizie kwamba, mimi
naahidi, siku ambayo kuna mmoja atakuwa jasiri wa kusema analeta suala la
Richmond hapa, mimi naahidi nitamuomba mheshimiwa Rais (John Magufuli)
anipumzishe uwaziri, ili niweze kuishughulikia hiyo kesi kiukamilifu iishe moja
kwa moja,” alisema Dk. Mwakyembe.
Alisema kamati
teule iliyoundwa na Bunge la Tisa kazi yake ilikuwa kuchunguza siyo kutoa
maamuzi. Alisema unapochunguza, suala la kusikiliza siyo lazima na ndiyo maana
kamati ilikuja bungeni na kuiwasilisha ripoti ikiwa na mashahidi zaidi ya 40
"wakitusubiri nje. “Aliyetakiwa kuhojiwa bungeni akajiuzulu, unamlaumu
Mwakyembe kwa hilo, naomba msipotoshe umma kuwa hakuhojiwa, ahojiwe vipi?
"Unajua ni
aibu, ni sawa na mtu anaenda mahakamani anasema unajua polisi hawakunipa haki
ya kuhojiwa “Polisi? Uko mahakamani... ndiyo pa kuhojiwa hapo, kwa hiyo ndugu
zangu mimi naomba tusipotoshe umma, sisi tulikuwa tumepata nyaraka za serikali
104, na tukahoji watu 75, tuliwauliza maswali 2,717 iko kwenye hansard.”
Alisema Kamati
haikuona sababu yoyote ya kumuhoji Lowassa kwa kuwa ilikuwa na ushahidi wote.“Mimi
niombe, mheshimiwa mwenyekiti (Andrew Chenge) kama kuna mtu yeyote hapa, bado
anakereketwa na kesi ya Richmond, aache maneno maneno hapa, leta hiyo kesi hapa
kama hatujawanyoa nywele kwa kipande cha chupa.”
Wakati Dk.
Mwakyembe akizungumza hayo, Kubenea aliomba utaratibu kwa Mwenyekiti akidai Dk.
Mwakyembe analiongopea bunge. Kubenea alisema Dk. Mwakyembe akiwa mwenyekiti wa
kamati hiyo alieleza kuwa mtu anaweza kujiuzulu kwa mambo mawili, moja kwa kuwa
yeye mwenyewe anahusika au mbili kwa kuwajibika kwa mambo yaliyofanywa na walio
chini yake.
Alisema Kwa
mujibu wa ‘hansard’ (kumbukumbu rasmi za bunge), Dk. Mwakyembe alisema Lowassa
alijiuzulu kwa mambo yaliyofanywa na walio chini yake lakini leo anasema ana
ushahidi wa asilimia 100 kwamba Lowassa alihusika na jambo hilo. “Mheshimiwa
Mwenyekiti naomba kwa idhini yako unipe muda niwasilishe hansard hapa kwenye
bunge hili kuthibitisha maneno ya Dk. Mwakyembe ya mwezi Februari mwaka 2008,”
alisema Kubenea.
Mara baada ya
Kubenea kueleza hayo, Dk. Mwakyembe alisema upinzani hawawezi kumsafisha
Lowassa kama madoa ya lami kwa kutumia kamba ya katani au maji, bali warudishe
bungeni suala hilo. Dk. Mwakyembe alimwomba Kubenea kuleta hoja ya Richmond
bungeni.“Ileteni hapa, naomba kwa Mungu mkiileta hapa nitafurahi kwasababu mimi
ninachosema hapa na ushahidi nilionao hapa... sisi tulimkuta huyu jamaa
amehusika."
Tupo hapa
kuthibitisha hilo suala naomba sana kwa sababu mmekuwa na makubaliano ya
kumsafisha, hamtaweza kumsafisha. Leteni kesi hapa.”
Dk. Mwakyembe pia
alijibu hoja iliyotolewa juzi na Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Peter Msigwa
kuwa mawaziri wa Serikali ya awamu ya tano ni waoga katika kumshauri Rais
Magufuli. Dk. Mwakyembe alisema hoja hiyo haina ukweli wowote na kwamba
mawaziri wa serikali ya awamu ya tano wanafanya kazi bila wasiwasi.
“Ohoo Mawaziri ni
waoga, hawana ujasiri, mimi nimekuwa najiuliza ni ujasiri wa aina gani? Wa
kumkaidi Waziri Mkuu, wa kumkaidi Rais, ujasiri upi?" Aliuliza.“Umeona
wapi ambapo mawaziri hawaongozwi na kanuni, ya kuwajibika kwa pamoja bungeni
katika mfumo wa bunge?"
No comments:
Post a Comment