TAASISI ya Tiba ya Moyo
ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa mara nyingine tena imefanya upimaji wa moyo wa
mtoto aliye tumboni mwa mama yake, kuchunguza magonjwa mbalimbali ya moyo.
Upimaji huo umefanywa
katika taasisi hiyo na Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo wa Watoto wa JKCI,
Naiz Majani.
Akizungumza na waandishi
wa habari, Dk. Naiz amesema kuna faida lukuki iwapo mjamzito ataamua kufanya
kipimo maalumu.
"Tunatumia Ultra
sound kama kawaida kufanya kipimo hiki, lakini inakuwa ina tofauti kidogo...
hatutumii mionzi yoyote, hivyo hakuna madhara anayoweza kuyapata mama au mtoto
wake aliye tumboni," amesema.
Ametaja
faida hizo kuwa ni kupunguza idadi ya vifo vya watoto wanaozaliwa na magonjwa
ya moyo, na kuwaondoa kwenye masumbufu wanayoweza kuyapata kutokana na
kuchelewa kupata matibabu.
"Kwa mara ya kwanza tuliwafanyia
kipimo hicho wajawazito 25 mwishoni mwa mwaka jana ambapo watano kati yao mimba
zao zilikutwa na matatizo.
"Wajawazito hao
wanatarajiwa kujifungua wakati wowote kuanzia sasa na watoto hao wataanza
kufuatiliwa kwa ukaribu na kupewa matibabu ya haraka," amesema.
Amesema waliamua kuanza
kufanya kipimo hicho baada ya kugundua watoto kadhaa hufikishwa katika taasisi
hiyo wakiwa katika hatua mbaya kiasi cha wao kushindwa kuwapatia matibabu.
Amesema inakadiriwa
katika kila watoto 100 wanaozaliwa nchini mmoja anakuwa amezaliwa
na magonjwa ya moyo.
"Mwaka jana
inakadiriwa walizaliwa watoto milioni moja, kwa msingi huo watoto wapatao
12,000 walizaliwa na magonjwa haya lakini tuliowaona kliniki yetu ni kati ya
700 hadi 750 pekee," amesema.
"Kuna baadhi ya
magonjwa ya moyo yanatakiwa kutibiwa mapema, lakini wanakuja umri umeshakwenda
tunashindwa kuwasaidia," amesema.
Mkurugenzi
wa JKCI, Profesa Mohamed Janabi amesema
dhumuni kubwa la kuanzisha huduma hiyo ni kugundua matatizo hayo mapema.
"Tunahamasisha
kina mama wajitokeze, Tanzania sasa imepiga hatua kubwa, tunafanya hivi kwa
sababu asilimia 85 ya wagonjwa tunaowafanyia upasuaji ni watoto.
"Na
hawa ndiyo tunaowategemea kuwa Taifa la kesho, tusipowagundua na kuwatibu
mapema maana yake ni kwamba watakuja kuwa mzigo kwa Taifa miaka ijayo,"
amesema.
Amefafanua
kwamba miaka ya nyuma si kwamba magonjwa ya moyo hayakuwapata watoto
bali hayakuweza kugundulika kutokana na uhaba wa wataalamu, vifaa.
"Watoto
wengi walikufa kwa kile kilichoelezwa ama ni typhoid, nimonia au surua, leo hii
wataalamu tupo, tulikwenda kujifunza kwa wenzetu katika nchi zilizoendelea ili
tuisaidie nchi yetu, magonjwa yote ya moyo yanatibika," amesisitiza.
No comments:
Post a Comment