Tunisia imesema Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu (AfCHPR)
ni lazima itangazwe kwa nguvu zote ili kuwawezesha wananchi barani Afrika
kufahamu uwepo wake, malengo ya kuanzishwa kwake pamoja na shughuli zake.
Akipokea ujumbe wa Mahakama hiyo katika Ikulu ya Tunisia, Rais wa Nchi
hiyo, Mh.Beji Caid Essebsi alipongeza uanzishwaji wa Mahakama hiyo na kuongeza kuwa inahakikisha ulinzi
wa Haki za Binadamu Barani Afrika.
“Kwa njia hii, Haki za
Binadamu Barani Afrika zitalindwa na kuhakikisha maendeleo endelevu ya
demokrasia kwa wananchi” Aliuambia ujumbe huo
uliohusisha majaji watatu akiwemo Rais wa AfCHPR, Jaji Sylvain Ore’.
Kwa upande wake Rais wa AfCHPR, Jaji Ore’ aliishukuru serikali ya
Tunisia kwa kukubali kuupokea ujumbe wake na kukutana na Viongozi na Maafisa
mbalimbali wa nchi hiyo na pia kuendesha semina kwa wadau mbalimbali nchini
humo kwa lengo la kuitangaza Mahakama.
Wakati wa ziara hiyo,Tunisia ilitia saini tamko la kuruhusu watu
binafsi na Mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) katika nchi hiyo
kupeleka kesi zao moja kwa moja katika Mahakama hiyo yenye Makao yake makuu
Jijini Arusha.
Hatua hiyo ya Tunisia ambayo ni utekelezaji wa kifungu cha 34 (6), Inalifanya
Taifa hilo kuwa Nchi ya nane Barani Afrika kukubali makundi hayo kupeleka kesi
katika Mamlaka za Mahakama hiyo.
Nchi nyingine ambazo ni Wanachama wa umoja wa Afrika zilizotoa tamko
kukubali Watu binafsi na NGO’s kutoka katika Nchi zao kupeleka kesi katika AfCHPR ni pamoja na: Benin,
Burkina Faso, Côte d’Ivoire, Ghana, Malawi, Mali
na Tanzania.
Utiwaji saini wa tamko hilo ulifanywa na Waziri wa mashauri ya kigeni
wa Tunisia, Mh.Khemaies Jhinaoui kwa niaba ya Serikali ya Nchi yake.
Rwanda ambayo hapo awali ilitia saini kukubali tamko hilo sasa imejitoa
ingawa Mkutano wa Kilele wa Viongozi wa Umoja wa Afrika uliofanyika Addis
Ababa, Ethiopia mapema mwaka huu uliitaka nchi hiyo kutafakari juu ya uamuzi
wake huo.
Kwa upande wake Misri ambayo haijaridhia itifaki iliyoanzisha Mahakama
ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu ilieleza kuridhishwa kwake na utekelezaji
wa shughuli za Mahakama hiyo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita na kuahidi
kuwa itaridhia itifaki husika.
Mahakama hiyo ilifanya ziara ya kikazi Nchini Tunisia na Misri kuanzia
April 9 hadi 14 Mwaka huu kwa lengo la kukuza uelewa wa wadau mbalimbali juu ya
uwepo ya Mahakama, Malengo yake na shughuli zake.
Tangu mwaka 2010, AfCHPR imefanikiwa kuendesha ziara 27 za kuelimisha
katika Maeneo mbalimbali Barani Afrika na kuendesha Semina na Mikutano ili
kukuza uelewa wa Masuala kuhusu ulinzi wa Haki za Binadamu Barani humo na
kuhamasisha Nchi wanachama wa AU kuridhia mkataba ulioanzisha Mahakama hiyo na
kutoa tamko la kuruhusu watu binafsi na NGO’s kupeleka kesi zao
Mahakamani hapo.
AfCHPR ilianzishwa na Nchi wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kwa mujibu
wa kifungu namba 1 cha itifaki ya Mkataba ya Mahakama hiyo na ilianza shughuli
zake rasmi Novemba, 2006 kwa lengo la kuimarisha Haki za Binadamu na Watu
Barani Afrika.
No comments:
Post a Comment