Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali bungeni
mjini Dodoma, Aprili 20, 2017.
Asisitiza vyombo vya dola vipewe muda wa kufanya uchunguzi wa matukio
ya kihalifu.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka
Watanzania kuendelea kuiamini Serikali yao na kuvipa muda vyombo vya dola
kuendelea kufanya uchunguzi dhidi ya matukio mbalimbali ya kihalifu yaliyotokea
nchini ili kubaini chanzo cha matatizo na wahusika.
Aidha, Waziri Mkuu ametoa wito kwa Watanzania
wote kuendelea na utamaduni wa kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa
taarifa pindi vinapotokea vitendo vya kihalifu au viashiria vyake katika maeneo
mbalimbali nchini.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Aprili 20, 2017) Bungeni mjini Dodoma katika kipindi cha maswali ya papo kwa
papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Kiongozi wa Kambi Rasmi ya
Upinzani Bungeni, Mheshimiwa Freeman Mbowe aliyetaka kupata kauli ya Serikali
juu ya hofu iliyotawala nchini kuhusu vitendo vya watu kuuliwa, kupotea na
kutekwa.
Waziri mkuu amesema “tukitoa taarifa mapema tunaweza kuharibu
upelelezi, tuviachie vyombo vetu vya dola viendelee kufuatilia kuona nani
anayesababisha vitendo hivyo na dosari iko wapi na nini chanzo chake alisisitiza,”.
Kadhalika Waziri Mkuu amewasii Watanzania
kuendeleza utamaduni mzuri wa watu kuheshimiana, kufuata kanuni na kuviachia
vyombo vya dola kutekeleza majukumu yake. “Moja ya majukumu ya
Serikali ni kuhakikisha Watanzania wanaishi kwa amani kwa kuwa na ulinzi wa
uhakika kwao wenyewe na mali zao wakati wote”.
Hata hivyo, Mheshimiwa Mbowe aliishauri
Serikali kushirikiana na vyombo vya kiuchunguzi vya kimataifa kuchunguza tukio
la kupotea kwa msaidizi wake Ben Saanane lililotokea miezi sita iliyopita,
ambapo Waziri Mkuu amesema kuwa Taifa lina mahusiano mazuri na mataifa
mbalimbali na inashirikiana nayo katika mambo mbalimbali likiwemo suala ya
ulinzi ambapo si rahisi kuainisha namna wanavyoshirikiana.
Waziri Mkuu ameongeza kuwa vyombo vyetu vina
weledi, vifaa na uwezo wa kutosha kufanya uchunguzi juu mambo yanayotokea
nchini hivyo amesisitiza wananchi kuendelea kuiamini kwani matukio haya ya
kihalifu likiwemo la mtu kutoweka au kufariki na haina kikomo cha uchunguzi,
mara zote uchunguzi unategemeana na aina ya tukio lenyewe au mazingira lilipo
tokea
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema
Serikali inafanya mapitio kwa vyama vyote vya Ushirika nchini kufuatia baadhi
ya vyama hivyo kuwa na mwenendo mbaya hali inayochangia upotevu wa fedha nyingi
na kukatisha tamaa wakulima.
Amesema hivi karibuni katika kikao cha wadau
wa zao la korosho kilichofanyika wilayani Bagamoyo Bodi ya Korosho ilidaiwa
kuhusika na ubadhilifu wa sh. bilioni 30 ambapo Serikali iliunda timu maalumu
ya uchunguzi na kubaini upotevu wa sh. bilioni sita na siyo sh. bilioni 30.
Hata hivyo amesema kwamba hasara hiyo ya sh.
bilioni sita haikusababishwa na bodi bali vyama vikuu na vya ushirikika
vilivyopo kwenye ngazi ya Kata na wilaya, ambavyo vyote vilifanyiwa uchuguzi na
hatua zimeanza kuchukuliwa.
Amesema matatizo hayo yako katika vyama vyote
vya ushirika hususan vya mazao ya Tumbaku, Kahawa, Pamba, Chai na mazao mengine
makuu, ambapo Serikali imeanza kupitia taarifa za ukaguzi kwa kina ili iweze
kufanya ukaguzi na sasa wanaendelea na uchunguzi wa chama kikuu cha tumbaku.
Waziri Mkuu amesema wakimaliza kufanya
uchunguzi katika chama kikuu cha tumbaku watachunguza vyama vingine vya pamba,
kahawa na chai lengo likiwa ni kuwalinda wakulima na kuhakikisha wanapata tija.
“Naomba kusisitiza hatua
zinaendelea kuchukuliwa na tutaendelea kuimarlisha na ushirika”.
Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu
swali la Mheshimiwa Mama Salma Kikwete aliyetaka kujua hatua zilizochukuliwa na
Serikali kuhusu ubadhirifu wa sh. bilioni 30 uliofanywa na Bodi ya Korosho
nchini.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisikiliza swali wakati
alipoulizwa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe (kulia), bungeni
mjini Dodoma, Aprili 20, 2017.
No comments:
Post a Comment