Tanga: MKUU wa Mkoa wa Tanga, Martin Shighella,
ameliagiza Shirika la Umeme Tanzania Tanesco Tanga, kuzikatia umeme taasisi
zote na mashirika ambayo yamelimbikiza madeni ya umeme.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini
kwake jana, Shighela alisema agizo la Rais Magufuli la kuzikatia umeme
mashirika na Taasisi za Serikali linapaswa kuheshimiwa hivyo kulitaka Shirika
hilo kuanza mchakato wa ukataji kwa wadaiwa sugu.
Alisema kuna baadhi ya Mashirika na
Taasisi zimekuwa zikilimbikiza madeni ya umeme ilhali zimekuwa na bajeti ya
umeme hivyo ili kujua umuhimu wa nishati hivyo ni kuzikatia.
“Natoa agizo kwa taasisi za Serikali na
Mashirika ya umma kuhakikisha wanalipa umeme kwa wakati na kuepuka
aibu ya kukatiwa, agizo la Rais linapaswa kuheshimiwa” alisema
Shighella na kuongeza.
“Rais ametoa agizo la kila mtumiaji wa
nishati ya umeme kulipa kwa wakati na yoyote ambaye analimbikiza madeni
kukatiwa, sisi ni watendaji kuhakikisha maagizo yake yatekelezwe” alisema.
Kwa upande wake Kaimu Meneja wa Tanesco
Tanga, Cesilia Msangi, amewataka watumiaji wa umeme Tanga kuhakikisha wanalipa
Ankara zao kwa wakati ili kuepuka kukatiwa umeme.
Alisema kwa sasa Shirika hilo linafanya
msako wa nyumba moja baada ya nyengine ikiwemo kuwabaini watu waliojiunganishia
umeme kwa njia za udanganyifu.
Alisema watu ambao watabainika kujipatia
umeme kwa njia za hila watafikishwa mahakamani wakiwemo mafundi vishoka ambao
wamekuwa wakilihujumu shirika hilo.
“Kuna baadhi ya watu wamekuwa wakirubuniwa
na wafundi vishoka kwa kuwaunganishia umeme, kwa hili hatutakuwa na msamaha
zaidi ya kuwafikisha mahakamani” alisema.
Aliwataka watumiaji wa umeme kuwa na ada
ya kulipa kwa wakati bili zao ili kuepuka malimbikizi ambayo unafika wakati
hushindwa kulipa na mwisho wake ni kukatiwa.
Kwa upande wake Meneja Mkuu wa kiwanda cha
Maziwa (Tanga Fresh) Michael Karata, amelitaka Shirika hilo kuwapunguzia
gharama za umeme kwa watu wenye viwanda.
Alisema gharama ya umeme ni kubwa hivyo
kulitaka kuwaangalia wawekezaji na wenye viwanda jambo ambalo litaweza kuongeza
ufanisi na uzalishaji wa bidhaa.
No comments:
Post a Comment