Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Mhe. Charles
Mwijage kulia akipokea cheti cha chanjo cha kimataifa kijulikanacho kama cheti
cha homa ya manjano kutoka kwa Afisa Afya Bw. Fadhili Kilamile mara baada ya
kupata chanjo hiyo leo kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma.
Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe. Mussa Zungu wa kwanza
kulia akisubiria kupewa cheti cha chanjo cha kimataifa kijulikanacho kama cheti
cha homa ya manjano kutoka kwa Kaimu Mkuu wa Kitengocha Afya Mipakani Bw.
Remidius Kakulu kushoto mara baada ya kupata chanjo hiyo leo kwenye viwanja vya
bunge mjini Dodoma.
Mbunge wa Viti Maalum jimbo la Singida Mhe. Martha
Mlatawa kwanza kulia akiandikiwa cheti cha chanjo cha kimataifa kijulikanacho kama
cheti cha homa ya manjano kutoka kwa Afisa Afya Agnes Shirima katikati mara baada
ya kupata chanjo hiyo leo kwenye viwanja vya bunge mjini Dodoma aliyesimama ni
Afisa Habari wa Wizara ya Afya Bi. Catherine Sungura.
Watanzania hususan wale wanaosafiri nje ya nchi zile zenye ugonjwa wa
homa ya manjano wanatakiwa kujitokeza kwenye vituo vilivyoainishwa na Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya kupata chanjo
hiyo pamoja na kubadilisha vyeti vipya.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji
Mhe.Charles Mwijage wakati alipofika kupata huduma ya chanjo ya homa ya manjano
ambayo inatolewa bungeni hapa.
Waziri Mwijage amesema duniani ugonjwa huu upo na zipo nchi nyingi
ambazo zimepoteza wananchi wake kwa kuugua ugonjwa huo “Suala hili ni muhimu
sana kwa afya zetu, pamoja na kwamba nchi yetu haina mgonjwa wa homa ya
manjano.
Aidha amesema maambukizi ya ugonjwa huu endapo mtu ataupata gharama za
matibabu yake ni ghali sana na inaweza kupelekea kupoteza maisha, hivyo ni
vyema kujitokeza kwa wingi kupata chanjo hiyo pamoja na kubadilisha kadi zao
kwani usiweke reheni maisha yako.
Hata hivyo aliwatahadharisha wafanyabiashara,wanafunzi wale wanaosafiri
au kusoma nje ya nchi ni vyema wahakikishe wanapata chanjo hiyo kuliko kupewa
kadi kwa njia nyingine kwani kadi hizi zimeboreshwa na zina alama za siri
ambazo nchi za kimataifa zina uwezo wa kusoma alama zetu.
Naye Mbunge wa Jimbo la Ilala Mhe.Mussa Zungu ameipongeza Wizara ya
Afya, maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kubadilisha kadi hizi
mpya kwa kuepukana na vyeti vingi ambavyo vilikua vinanunuliwa mtaani bila
kupata huduma za kupata chanjo,hivyo ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha
wanapata chanjo hizo kwani ilikua ni hatari sana hususan nchi zile zenye
milipuko wa homa za manjano na hivyo kupata vyeti ambavyo ni halali.
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto limeongeza
muda wa kubadilisha vyeti vya zamani hadi mwisho wa mwezi huu na baada ya hapo
vyeti vya zamani havitatambulika tena.
No comments:
Post a Comment