Ni mwendo wa ‘toa kitu weka kitu’.
Baada ya Aishi Manula kusaini mkataba wa miaka miwili kujiunga na Simba, klabu
ya Azam imemnasa golikipa wa Mbao FC Benedict Haule na kumsainisha mkataba
wa miaka miwili ili kuziba nafasi iliyoachwa na Manula.
Haule amepata umaarufu baada ya
kusimamishwa kwa aliyekua golikipa namba moja wa Mbao Musa Ngwegwe. Haule
alifanya vizuri kwenye mechi alizosimama golini kuelekea mwisho mwa msimu na
kuisaidia timu yake kukwepa kushuka daraja huku akiifikisha fainali ya Azam
Sports Federation Cup.
Mechi kati ya Mbao dhidi ya vigogo vya
soka nchini (Simba na Yanga) zilimpa jina baada ya kuonesha kiwango cha juu.
Licha ya kupoteza mchezo kwa mabao 3-2 mbele ya Simba, kipa huyo alikuwa kwenye
kiwango bora.
Alionesha uwezo mkubwa kwenye mchezo
wa mwisho wa ligi dhidi ya Yanga na kuiongoza Mbao kushinda kwa goli 1-0
ushindi ambao uliwahakikishia kubaki kwenye ligi kuu kwa ajili ha msimu ujao.
Simba watamkumbuka Haule kwa kile
alichokifanya kwenye uwanja wa Jamhuri Dodoma siku ya mechi ya fainali ya Azam
Sports Federation Cup ambapo Simba ilishinda kwa magoli 2-1 na kuchukua taji
hilo lililowapa fursa ya kucheza michuano ya Caf Confederation Cup msimu ujao.
Haule amesaini mkataba wa miaka miwili
leo jioni mbele ya Meneja Mkuu wa Azam FC, Abdul Mohamed sambamba na Meneja wa
timu, Phillip Alando, utakaoanza kufanya kazi kuanzia Julai Mosi mwaka huu.
Usajili huo unamfanya kipa huyo
kurejea tena nyumbani ndani ya viunga vya Azam Complex, kwani aliwahi kulelewa
katika kituo cha Azam Academy chini ya Kocha wa Makipa wa Azam FC, Idd
Abubakar.
Kipa huyo anaungana na makipa wengine
wa Azam FC, Mwadini Ally na Metecha Mnata, tayari kabisa kuanza mchakamchaka wa
kujiandaa na msimu ujao kuanzia Julai 3 mwaka huu.
Huo ni usajili wa nne kwa Azam FC
kuelekea msimu ujao 2017/2018, wengine ambao tayari saini zao zimenaswa ni
kiungo nyota Salmin Hoza na washambuliaji wanaokuja kwa kasi Mbaraka Yusuph na
Wazir Junior.
Mbali na usajili wa wachezaji hao,
tayari benchi la ufundi la mabingwa hao wa Kombe la Mapinduzi na Ngao ya Jamii
chini ya Mromania Aristica Cioaba, limefanya uamuzi wa kuwapandisha vijana sita
kutoka kituo cha Azam Academy.
Mabeki Abbas Kapombe, Abdul Omary,
Godfrey Elias na Ramadhan Mohammed, anayemudu kucheza namba nyingi uwanjani,
kiungo Stanslaus Ladislaus na mshambuliaji Yahaya Zaid, aliyeibuka mfungaji
bora wa Ligi Daraja la Kwanza msimu uliopita kwa mabao yake tisa wakati
alipokuwa akiichezea kwa mkopo Ashanti United.
No comments:
Post a Comment