Mwana wa Gaddafi Saif al-Islam aachiliwa huru Libya - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, June 12, 2017

Mwana wa Gaddafi Saif al-Islam aachiliwa huru Libya

Saif al-Islam Gaddafi (katika picha hii iliyopigwa mwaka 2011 baada ya kukamatwa) alihukumiwa kifo mjini Tripoli mwaka 2015

Saif al-Islam Gaddafi, mwana wa pili wa aliyekuwa kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi anadaiwa kuwa huru baada ya kuzuiliwa kwa kipindi cha miaka sita.

Kuna wasiwasi huenda hatua hiyo ikatikisa zaidi hali ya kisiasa na kiusalama nchini Libya.

Saif al-Islam anadaiwa kuachiliwa huru baada ya kupewa msamaha.

Ndiye aliyependelewa na babake kuwa mrithi wake na amekuwa akizuiliwa na kundi la wanamgambo katika mji wa Zintan kwa miaka sita.

Wanamgambo hao wa Abu Bakr al-Siddiq Battalion walisema aliachiliwa huru Ijumaa lakini bado hajaoneshwa hadharani.

Taarifa nchini Libya zinasema kwa sasa amo katika mji wa Bayda, mashariki mwa Libya, kwa jamaa zake.

Wanamgambo hao wanadaiwa kumuachilia huru baada ya ombi kutoka kwa "serikali ya muda".

Serikali hiyo - yenye makao yake mashariki mwa nchi hiyo - ilikuwa tayari imetoa msamaha kwa Saif al-Islam.

Hata hivyo, alikuwa amehukumiwa kifo na mahakama mjini Tripoli, magharibi mwa nchi hiyo bila yeye kuwepo mahakamani.

Maeneo ya magharibi yanatawaliwa na serikali inayopingana na serikali ya mashariki mwa Libya, lakini serikali hiyo ya magharibi yenye makao yake makuu Tripoli ndiyo inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.

Kwa kirefu, inafahamika kama Serikali ya Mwafaka wa Kitaifa.


Taarifa zilizowahi kutolewa awali kuhusu kuachiliwa kwa Saif al-Islam Gaddafi baadaye zilibainika kuwa na uongo.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages