Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inapenda kutoa maelekezo kufuatia malalamiko kuhusu ulipaji wa ada na malipo mengine kwa shule za Msingi na Sekondari zisizo za Serikali zitakapofunguliwa baada ya janga la Corona. Wizara inaelekeza na kusisitiza kuwa wanafunzi wote wapokelewe kwa ajili ya kuendelea na masomo ifikapo tarehe 29/06/2020.
Kulingana na ratiba iliyotolewa na Wizara, wanafunzi wanatarajiwa kukamilisha masomo kama inavyoelekezwa na Mihtasari ya madarasa waliyopo. Hivyo, ada za shule zilipwe kulingana na makubaliano yaliyoafikiwa mwanzoni mwa mwaka wa masomo. Wizara inaendelea kusisitiza maelekezo ya awali kwamba kusiwepo na nyongeza yoyote katika kiwango cha ada.
Wazazi pia wanatakiwa kuzingatia kuwa kiwango cha ada huwa kinakadiriwa kwa kuzingatia gharama mbalimbali za uendeshaji wa shule, gharama ambazo ziliendelea kuwepo hata muda ambao shule zilikuwa zimefungwa. Gharama hizi ni pamoja na mishahara ya watumishi, ankara za umeme na maji, n.k.
Aidha, kwa upande wa malipo ya chakula na usafiri, Wizara inazielekeza Kamati/Bodi za Shule kufanya uchambuzi wa gharama inayopaswa kupungua kwa siku ambazo wanafunzi hawakuwa shuleni. Tathmini hii izingatie ratiba mpya ya mihula iliyotolewa na Wizara.
Kulingana na Sheria ya Elimu, Sura Na. 343 (RE 2002), uendeshaji wa shule unasimamiwa na Kamati/Bodi za Shule, vyombo ambavyo vimeundwa kwa mujibu wa Sheria hiyo. Hivyo, wamiliki wa shule wanaelekezwa kuzingatia Sharia hiyo na kuzipa nafasi Bodi/Kamati za Shule kutekeleza majukumu kulingana na Sheria iliyoziunda.
Kwa kuzingatia kwamba Serikali ilifunga shule wakati muhula wa masomo ukiwa unaendelea, Wizara inaelekeza kwamba wanafunzi wote WAPOKELEWE na kuendelea na masomo yao bila kikwazo chochote ili kukamilisha muhula huo.
Kwa mara nyingine tena Wizara inapenda kutoa shukrani kwa wamiliki wote wa shule zisizo za Serikali kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha katika utekelezaji wa majukumu yao ya utoaji wa elimu kwa watoto wa kitanzania.
No comments:
Post a Comment