Serikali Yaipongeza CRDB Bank Foundation Kuwawezesha Kiuchumi Vijana Na Wanawake Wajasiriamali Nchini - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Monday, June 3, 2024

Serikali Yaipongeza CRDB Bank Foundation Kuwawezesha Kiuchumi Vijana Na Wanawake Wajasiriamali Nchini

Mkurugenzi wa Jinsia wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Badru Abdunuru aliyekuwa mgeni rasmi katika hafla ya mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 150 Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi ya Data Sustainable Development Organization, Sihaba Madenge ambazo ni mtaji wezeshi kwa baadhi ya wanachama wa asasi hiyo waliokidhi vigezo vya Programu ya Imbeju inayotekelezwa na Taasisi ya CRDB Bank Foundation. Wanaoshuhudia ni Mkurugenzi Mtendaji wa BUTA Vicoba, Semeni Gama (wa kwanza kushoto), Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa (wa pili kushoto, Meneja wa Kanda ya Mashariki wa Benki ya CRDB, Badru Iddi (wa nne kulia), Mkuu wa Kitengo cha Kuendeleza Biashara Changa wa CRDB Bank Foundation, Fadhil Bushagama (wa kwanza kulia) pamoja na wanachama wa Asasi ya Data Sustainable Development Organization.

Dar es Salaam: Serikali imeipongeza Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kutoa mafunzo ya ujasiariamali na elimu ya fedha pamoja na mitaji wezeshi zaidi ya shilingi bilioni 10 kwa vijana na wanawake wajasiriamali nchini.

Pongezi hizo zimetolewa na Mkurugenzi wa Jinsia wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Badru Abdunuru wakati wa hafla ya mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya fedha pamoja na kukabidhi mitaji wezeshi ya jumla ya kiasi cha shilingi milioni 150 kwa wanachama wa Asasi ya Data Sustainable Development ya Dar es Salaam. Katika mafunzo hayo, ilibainishwa kuwa kati ya shilingi bilioni 10 za mtaji wezeshi zilizotolewa mpaka sasa, wakazi wa Dar es Salaam wamepokea zaidi ya shilingi bilioni 3.6.
Abdunuru amesema ni ukweli wa dhahiri kuwa wanawake na vijana ndio injini ya uchumi kwani wana uwezo mkubwa wa kuliinua taifa kiuchumi. Kwa kuzingatia Ripoti ya Sensa na Makazi ya mwaka 2022, amesema asilimia 51 ya watu wote nchini ni wanawake na asilimia 75 ni vijana hali inayodhihirisha umuhimu wa kundi hili kwa nguvukazi ya taifa.

Hata hivyo, wanawake na vijana wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwamo mila na desturi kandamizi, elimu duni, ukosefu wa mitaji na stadi za ujasiriamali. Tukizitambua changamoto hizi, serikali imechukua hatua mbalimbali zinazolenga kujenga uchumi jumuishi na shirikishi ili kuwakomboa kiuchumi,” amesema Abdunuru.

Aliongezea kuwa, “Tunaendelea kufanya kazi kwa bidii kufikia malengo ya Jukwaa la Kimataifa ya Kukuza usawa wa Kijinsia hususan katika haki na usawa wa kiuchumi. Nawapongeza Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kuja na ubunifu huu unaounga mkono jitihada za serikali kuwakomboa kiuchumi vijana na wanawake.
Ili kuwawezesha zaidi wajasiriamali wanawake na vijana, Mkurugenzi huyo amesema ni muhimu kwa wadau wote wa maendeleo wakashiriki mkakati huu kwani serikali pekee haitoweza kutatua changamoto zote zilizopo.

Niipongeze CRDB Bank Foundation kwa kuja na programu hii ambayo inalenga kuboresha maisha na kuimarisha biashara za vijana na wanawake kwa kuwapa mafunzo na ushauri wa namna bora ya kusimamia na kuendesha biashara zao, pamoja na kuwapa mitaji wezeshi. Naamini mmefungua milango kwa taasisi nyingine kubuni namna zinavyoweza kuyashirikisha makundi haya katika mipango yao,” amesema Abdunuru.
Akizungumza kwenye mafunzo hayo, Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma wa Benki ya CRDB na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Mwambapa amesema mpaka mwishoni mwa Mei wameshatoa mafunzo kwa zaidi ya wanawake na vijana 400,000 ambao baadhi yao wamenufaika na mitaji wezeshi yenye thamani ya shilingi bilioni 10.

Uwezeshaji huu umefanyika kupitia madirisha mbalimbali yaliyo chini ya programu yetu ya Imbeju ikiwamo Imbeju Ng’ara ambalo limejielekeza kuwawezesha wanawake, Imbeju Buni kwa ajili ya vijana wenye biashara changa, na Imbeju Kilimo linalowasaidia wakulima wadogo pembejeo na zana za kilimo pamoja na kuwalinda kupitia bima ya maisha na mazao. Vilevile, tuna Imbeju Nishati Safi, dirisha linalotoa elimu na kuhamasisha matumizi ya nishati safi kwa mama lishe,” amesema Tully.

Mafanikio hayo, Tully amesema yasingeweza kufikiwa bila kuwashirikisha wabia wao wa kimkakati kama ilivyo Asasi ya Data Sustainable Development yenye zaidi ya wanachama 1,800 na wengine wengi kuanzia mashirika ya kimataifa, taasisi za serikali na vikundi vya wanawake wajasiriamali.
Katika zaidi ya shilingi bilioni 10 tulizozitoa nchini kote kama mtaji wezeshi kwa wajasiriamali, shilingi bilioni 3.6 tumezitoa kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam na leo tunajivunia kutanua wigo wa wanufaika kwa kutoa mitaji wezeshi kwa wanachama wa Asasi ya Data Sustainable Development ambao tumeingia nao mkataba wa ushirikiano hivi karibuni,” amesema Tully wakati wa kuakikabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 150 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa asasi hiyo, Sihaba Madenge.

Akipokea mfano wa hundi hiyo kwa ajili ya wanachama wake, Sihaba amesema ubunifu wa CRDB Bank Foundation ni wa kipekee kwani umeliona kundi kubwa ambalo ni muhimu ila lenye vikwazo vingi kupata huduma za fedha hasa mikopo ya kukuza biashara zao.

Wanawake wengi wanapambana na maisha kuhakikisha wanazihudumia familia zao kwa kufanya biashara ndogondogo. Kikwazo kikubwa kwao ni mtaji kwani wengi hawana dhamana zinazohitajika katika benki nyingi hivyo kujikuta wakikwama kwa muda mrefu. Fursa hizi za kupata mtaji wezeshi kupitia Programu ya Imbeju bila masharti yoyote hakika ni ukombozi wa kiuchumi kwa wanawake wengi tunaipongeza na kuishukuru sana Taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa ubunifu huu,” amesema Sihaba.

Mkurugenzi huyo pia ameiomba CRDB Bank Foundation kupeleka fursa za Programu ya Imbeju mpaka vijijini waliko wanawake wengi kwani kuna mwamko mkubwa wa wanawake kujishughulisha kiuchumi japo suala la upatikanaji wa mitaji linawakwamisha wengi.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages