Rais Mstaafu na Mjumbe Maalum wa Kamisheni ya Kimataifa ya Kugharamia
Fursa za Elimu Duniani Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amekamilisha ziara yake ya
kuhamasisha utekekezaji wa Ripoti ya Kamisheni hiyo ijulikanayo kama 'Kizazi
Cha Elimu' (The Learning Generation).
Katika ziara hiyo iliyomfikisha katika nchi 15,
Rais Mstaafu Kikwete amekutana na Wakuu wa Nchi 12 wa nchi za Uganda, Malawi,
Msumbiji, Congo, Tunisia, Ghana, Chad, Gabon, Ivory Coast, Namibia, Afrika
Kusini na Botswana. Aidha amekutana na Makamu wa Rais wa Nigeria na Mawaziri
Wakuu wa Ethiopia na Tanzania. Pamoja na viongozi wa nchi na Serikali, Rais
Mstaafu amekutana na viongozi wa Taasisi za Kikanda 3 ambao ni
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AUC), Rais wa Benki ya Maendeleo ya
Afrika (AfDB) na Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC).
Madhumuni ya ziara hizo yalikuwa ni kufikisha
ujumbe wa Kamisheni na Ripoti yake juu ya umuhimu wa nchi za uchumi wa kati na
chini (low and middle income countries) kufanya mapinduzi makubwa ya elimu ili
kukabiliana na janga kubwa la elimu linaloinyemelea dunia.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamisheni hiyo, ubora wa
elimu inayotolewa na nchi zinazoendelea za uchumi wa kati na chini ni ile
ambayo imetolewa na nchi zilizoendelea miaka 70 iliyopita. Aidha, nchi
zinazoendelea ziko nyuma sana katika vigezo vitatu muhimu vya elimu vya fursa ya kujiunga
na elimu (access to education), kumaliza elimu (completion) na ufaulu na
kuelimika (learning outcomes).
Vile vile, Ripoti ya Kamisheni inaonyesha kuwa
Barani Afrika ni asilimia 5 tu ndio wenye elimu ya Chuo Kikuu na asilimia 20
ndio wenye Elimu ya Sekondari jambo ambalo linafanya bara la Afrika kuwa 'Bara
la Wahitimu wa Elimu ya Msingi'. Hali hii ni ya kukatisha tamaa wakati ambapo
nchi za Asia za Japan, Korea Kusini na Thailand zikitazamia kufikia lengo la
asilimia 80 ya wanafunzi wake kujiunga na elimu ya Chuo Kikuu ifikapo mwaka
2050. Barani Afrika, inatarajiwa kufikia asilimia 15 tu ya wanafunzi wake,
ambapo asilimia 10 kati ya hiyo ni Afrika ya Kaskazini na Afrika Kusini mwa Jangwa
la Sahara kubakia na asilimia 5 tu.
Kamisheni inatahadharisha kwamba endapo hatua za
makusudi hazitachukuliwa, inakisiwa kuwa ifikapo mwaka 2030, watoto milioni 160
barani Afrika watakuwa nje ya mfumo wa Elimu wakati ambapo, Dunia imeazimia
kupitia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kuwa ifikapo mwaka 2030 pasiwepo
na mtoto aliyeachwa nyuma. Aidha, stadi zinaonyesha kuwa mapinduzi ya
teknolojia yatafuta ajira zipatazo bilioni 2 duniani ambapo asilimia 70 ya
ajira hizo ziko barani Afrika. Bila kuwekeza katika Elimu, Bara la Afrika
halitakuwa na nafasi huko tuendako.
Kamisheni inapendekeza nchi zinazoendelea kufanya
mageuzi katika mifumo yao ya elimu kwa kufanya yafuatayo:
1. Kuongeza Ufanisi kwa kuhimiza usimamizi mzuri na
kuziba mianya ya rushwa na upotevu katika mfumo wa elimu;
2. Kupanua fursa za elimu kwa kuhakikisha kila
mtoto anapata elimu bila kujali jamii anayotoka, jinsia au ubaguzi wa aina
yoyote;
3. Matumizi ya Teknolojia na mbinu bora za kitafiti
za utoaji wa elimu ikiwemo kuainisha mitaala iendane na mabadiliko ya dunia; na
4. Kuongeza uwekezaji wa fedha katika elimu ili
kuwezesha utoaji wa elimu bora yenye kukidhi viwango na mahitaji ya sasa na
baadae.
Katika ziara yake katika nchi 14 zilizochaguliwa
kuongoza mapinduzi ya elimu (Pioneer Countries) za
Botswana, Chad, Congo, Ethiopia, Gabon, Ghana, Ivory Coast, Malawi, Msumbiji,
Nigeria, Namibia, Tanzania, Tunisia na Uganda, Rais Mstaafu Kikwete ameridhishwa
na jitihada na utashi wa hali ya juu unaoonyeshwa na viongozi na serikali zao
katika kupanua fursa za elimu na kuinua hali ya elimu ya watoto wao.
Changamoto
kubwa iliyoainishwa ni uwezo mdogo wa serikali hizo kugharamia kikamilifu fursa
za elimu. Tayari nchi hizo zinatumia wastani wa asilimia 18 hadi 20 wa bajeti
zao katika elimu, na bajeti ya elimu ni kubwa katika nchi zote alizotembelea.
Imejidhihisha kuwa ni vigumu kwa nchi hizi kuvuka ukomo wa bajeti huo bila
kupata chanzo kingine cha fedha nje ya bajeti zao.
Kwa ajili hiyo, Kamisheni inaendelea na jitihada
zake za kushawishi Jumuiya ya Kimataifa kuongeza misaada na fedha za mikopo
kugharamia elimu katika nchi zinazoendelea. Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamisheni,
fedha za wahisani katika elimu zimekuwa zikipungua kutoka asilimia 13 mwaka
2003 hadi asilimia 10 mwaka 2013. Aidha, stadi imeonyesha kuwa fedha za elimu
zimekuwa zikipungua wakati ambapo fedha kwa ajili ya miundombinu na afya
zimekuwa zikiongezeka.
Kamisheni ya Elimu inaendelea na jitihada za
kushawishi nchi wahisani, mashirika ya fedha ya kimataifa na washirika wa
maendeleo kuongeza fedha na uwekezaji katika elimu kwa manufaa ya dunia na
kizazi kijacho. Lengo ni kushawishi ongezeko la misaada katika elimu (ODA)
kufikia asilimia 15 na fedha za mikopo kufikia walau asilimia 0.5 ya
GDP zao ambayo ni sawa na dola za kimarekani bilioni 50 ifikapo mwaka 2030.
Kwa ajili hiyo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete
amejumuika na Mwenyekiti wa Kamisheni ya Kimataifa ya Elimu Mheshimiwa Waziri
Mkuu wa Uingereza Mstaafu Gordon Brown kukutana na Mawaziri wa Fedha wa nchi 14
na Wakuu wa Mashirika ya Fedha pembezoni mwa Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia
unaondelea jijini Washington D.C. kushawishi kutekelezwa kwa azma hiyo.
No comments:
Post a Comment