Hatimaye Vijana Yatima Wapata Haki yao ya Kurithi Mali - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Friday, February 1, 2019

Hatimaye Vijana Yatima Wapata Haki yao ya Kurithi Mali

Bi. Prepetua Buzima (Kushoto), Mama Mdogo wa Vijana wawili--Samson Kuhali (20) na Mashaka Kuhali (17) akiongea na Mwanamke aliyenunua nyumba iliyokuwa na mgogoro wa Mirathi uliyohusisha vijana hao wawili na baba yao mlezi. Mwanzoni baba mlezi aligoma kabisa kuwapa vijana haki yao ya mirathi, lakini baadae walifanikiwa kupata haki yao baada ya kusaidiwa na wasaidizi wa kisheria Wilaya ya Mbogwe--Geita.
Kwa miaka mingi, maelfu ya wajane na watoto wa kike wamekuwa wakinyimwa haki zao za kurithi mali baada ya kifo cha baba mzazi katika familia nyingi nchini Tanzania. Ingawa kesi nyingi haziripotiwi, kuna matukio mengi ya wajane na wasichana wanaofukuzwa nyumbani na kunyimwa haki yao ya kurithi mali.
Hata hivyo, mambo yamebadilika kwani watoto wa kiume nao wanakumbana na matatizo kama hayo ya kunyimwa haki zao baada ya kufariki kwa wazazi wao.
Vijana hao—Samson Kuhali (20) na Mashaka Kuhali (17) —wa Kijiji cha Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe (Geita)—ni mifano hai ya vijana wa kiume, ambao wamekuwa wakinyanyasika na kufukuzwa nyumbani baada ya kifo cha mama yao.
Kabla ya kifo cha mama yao, vijana hao walikuwa wakiishi kwa amani na mama yao na baba mlezi katika nyumba moja (iliyojengwa kwa ushirikiano wa baba na mama yao), ambayo iko Kijiji cha Masumbwe, Wilaya ya Mbogwe. Familia iliishi kwa amani na mapatano.
Lakini hali ilibadilika sana baada ya kifo cha mama yao. Baba mlezi alianza kuwatesa kwa kuwanyima haki zao za msingi, ikiwemo ya kupata mahitaji yao ya kila siku. Baadaye aliwafukuza watoto hao wawili nyumbani kwa kisingizio kwamba hawana haki ya kurithi mali.
Wakiongozwa na Bi Perepetua Ruben Buzima, ambaye ni mama yao mdogo, ndugu walijitahidi sana kudai nyumba irudishwe na kuhakikisha watoto hao wawili wanapata haki yao ya mirathi. Walitumia fedha na muda mwingi wa kufuatilia kesi kwa namna mbalimbali, lakini jitihada zao hazikuzaa matunda kwani baba mlezi aliendelea kuwanyima vijana hao haki zao.
Ndugu wa marehemu walienda kwa Ofisi ya Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mbogwe, ambapo walishauriwa kufungua kesi Mahakama ya Mwanzo ya Masumbwe. Baba mlezi aliitwa na mahakama, lakini hakuonekana mahakamani. Ndugu wa marehemu waliruhusiwa na mahakama kuchagua msimamizi wa mirathi (nyumba). Wanafamilia walikaa na kumteua Bw Raphael Ruben (50) kuwa msimamizi wa mirathi. Hata hivyo, baba mlezi hakutoa ushirikiano. Alienda tena mahakama ya mwanzo kupeleka shauri, ambapo hakimu alishindwa kutatua mgogoro uliokuwepo. Familia ilimtafuta mwanasheria aliyekubali kusaidia, lakini kwa gharama, ambayo wanafamilia walishindwa kuimudu.
Baadhi ya wanakijiji waliishauri familia kupata ushauri kutoka kwa wasaidizi wa kisheria. Walikutana na msaidizi wa kisheria kutoka Wilaya ya Mbogwe aliyekubali kuwasaidia kwa kuandaa na kukata rufaa kwa Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya ya Mbogwe. Baraza la Ardhi ma Nyumba la Wilaya lilimwita baba mlezi, lilisikiliza utetezi wa pande zote mbili na kuamuru nyumba iuzwe kwa bei ya soko na fedha zitakazopatikana zigawanywe kwa usawa kwa pande zote mbili (watoto wa kiume wawili na baba yao mlezi).
Hatimaye, nyumba iliuzwa kwa Sh2.5 milioni na fedha zilizopatikana ziligawanywa kama Baraza lilivyoagiza. Vijana hao wawili wamehamia kijiji kingine, ambapo kwa sasa wanajishughulisha na biashara ndogo ndogo na kupata riziki zao.
“Kabla ya msaidizi wa kisheria kuingilia kati kwenye huu mgogoro wa mirathi, sisi (familia) tulitumia fedha, nguvu na muda mwingi katika kesi hii—kwa kuandaa hati za kimahakama na gharama zake. Ilikuwa rahisi baada ya msaidizi wa kisheria kuingilia kati na kusaidia na baada ya muda mfupi, kesi iliisha na vijana hao kupata haki yao,” anasema Bi Perepetua Buzima, ambaye ni mama mdogo wa vijana hao.
“Tunashukuru kwamba haki imetamalaki. Vijana hawa wawili wamepata haki yao na sasa wanajishughulisha na biashara ndogo ndogo. Sasa naelewa umuhimu wa kuandika wosia kulinda familia zetu, hasa mke na watoto, kutokana na matatizo wanayoweza kukumbana nayo baadaye,” anasema Bi Julie Mozao, rafiki wa familia.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages