DKT.DIMWA: ASEMA CCM INATHAMINI MCHANGO WA CPC KISIASA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Wednesday, December 4, 2024

DKT.DIMWA: ASEMA CCM INATHAMINI MCHANGO WA CPC KISIASA

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa, akizungumza na Viongozi Wandamizi wa Chama Cha Kikomunisti cha China (CPC) waliofika Ofisini kwake Kisiwandui Zanzibar kwa ajili ya mazungumzo ya kuimarisha taasisi hizo mbili.

Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

NAIBU Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,amesema chama hicho kitaendelea kuthamini na kuendeleza kwa vitendo mahusiano mema ya kisiasa, kijamii na kiplomasia baina yake na chama cha kikomunisti cha China (CPC).

Hayo ameyasema wakati akizungumza na ujumbe wa Viongozi wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) wa Kanda ya Afrika waliofika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar, ambapo mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano baina ya vyama hivyo viwili vya kisiasa.

Dkt. Dimwa alisisitiza kwamba CCM itaendelea kusimamia kwa vitendo mahusiano yake na CPC, akieleza kuwa ushirikiano huu utasaidia kuimarisha nyanja za kijamii, kisiasa, na kidiplomasia kwa maslahi ya wananchi wa pande zote mbili.

Aliendelea na kusisitiza kuwa ushirikiano wa CCM na CPC utaleta manufaa kwa maendeleo ya Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

"CCM itaendeleza na kusimamia kikamilifu mahusiano yetu na CPC ili kuimarisha maendeleo katika nyanja za kijamii, kisiasa, na kidiplomasia, na kuhakikisha kuwa wananchi wa pande zote mbili wanapata faida ya ushirikiano huu," alisema Dkt. Dimwa.

Aidha, Dkt. Dimwa aliomba CPC kuangalia uwezekano wa kusaidia CCM Zanzibar katika kujenga chuo cha kisasa cha uongozi cha Vijana kilichopo katika kijiji cha Tunguu, akisisitiza kuwa chuo hicho kitakuwa na mchango mkubwa katika kukuza uongozi wa vijana na kuwaandaa kuwa viongozi wa baadaye.

Aliongeza kuwa kupitia ziara hii, pande zote mbili zitabadilishana uzoefu na mawazo kuhusu ushirikiano wa kibiashara, ambapo Zanzibar itakuwa na fursa ya kuuza bidhaa zake kama karafuu na viungo (Spaces) nchini China, huku China nayo ikileta bidhaa zake Zanzibar.

Dkt. Dimwa pia alizungumzia maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, akisema kuwa CCM imejipanga vyema na itapata ushindi mkubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa ilani yake, ambayo imekidhi mahitaji ya wananchi.

Aliomba CPC kuendelea kutoa msaada katika kuendeleza programu za kuwajengea uwezo wa kitaaluma na ujuzi viongozi na watendaji wa CCM ili waweze kuendana na mahitaji ya kisiasa ya zama za sasa.

Akizungumzia mchango wa China kwa Zanzibar, Dkt. Dimwa alikumbuka mchango wa Rais wa China, Mao Zedong, ambaye alifanya kazi kwa karibu na Rais wa kwanza wa Zanzibar, Marehemu Abeid Amani Karume, katika kuijenga Zanzibar na kutambua Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964.

Aliongeza kuwa serikali ya China imekuwa ikisaidia katika sekta za elimu, afya, uvuvi, miundombinu, na kuwajengea uwezo wajasiriamali wadogo wadogo kupitia mafunzo na zana za kisasa.

Pia, alitoa shukrani kwa China kwa msaada wake katika ujenzi wa Chuo cha Kisasa cha Uongozi cha Mwl. Nyerere cha Kibaha, kinachotoa mafunzo ya elimu ya juu ya masuala ya uongozi na fani mbalimbali kwa watendaji wa Chama,Serikali,sekta binafsi na wananchi kwa ujumla.

Dkt. Dimwa alisisitiza kuwa dhamira ya serikali ya Zanzibar chini ya Rais Dkt. Hussein Mwinyi ni kuhakikisha kila mwananchi anapata maisha bora na kwamba kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar inaendelea kuimarika kwa nguvu.

Naye Naibu Mkuu wa Ofisi ya Kanda ya Afrika katika Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara na Kiongozi wa Idara ya Kimataifa ya Kamati Kuu ya CPC, Cde. Liang Anping, alisema kuwa CPC na China wanajivunia kuwa na mahusiano imara na serikali ya Tanzania na Zanzibar.

Alisisitiza kuwa CPC itaendelea kutoa ushirikiano wa dhati kwa Zanzibar kupitia Tanzania, hasa katika kuimarisha mafunzo ya uongozi na mipango endelevu ya kukuza uchumi wa Zanzibar.

Cde. Liang alieleza kuwa serikali ya China imejizatiti kuunga mkono juhudi za maendeleo za nchi za Afrika, hasa Tanzania, na kuhakikisha zinajitegemea kiuchumi.

Aliongeza kuwa China inaridhishwa na maendeleo ya Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Rais Dkt. Hussein Mwinyi, ambao wamefungua milango ya uwekezaji na diplomasia kwa manufaa ya nchi zote mbili.

"China itaendelea kutoa fursa za kubadilishana ujuzi na uzoefu kwa wataalamu wa fani mbalimbali. Mapendekezo, ushauri, na maombi yaliyowasilishwa yatafanyiwa kazi kwa vitendo," alisisitiza Cde. Liang.

Aidha, Cde. Liang aliongeza kuwa Zanzibar ina mazingira mazuri ya uwekezaji na inavutia wawekezaji kutokana na sera za China kiuchumi, na kwamba baada ya ziara hii, wanatarajia kuimarisha ushirikiano na Zanzibar kwa manufaa ya pande zote mbili.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages