Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akizungumza na wananchi wa Kibaoni, katika Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akiwa na ni mke wake, Mary Majaliwa (kushoto), akizungumza na
wananchi, wakati alipokagua kituo cha Afya Kibaoni, katika Wilaya ya Kilombero,
mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akitembelea wagonjwa, kwenye Kituo cha Afya Kibaoni, kilichopo katika
Wilaya ya Kilombero, mkoani Morogoro.
Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa, akiwa na Daktari Mkuu wa Kituo cha Afya Kibaoni, Happiness Ndosi
(kushoto), akikagua kituo hicho, kilichopo katika Wilaya ya Kilombero,
mkoani Morogoro.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupeleka gari la kubebea
wangonjwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni kilichopo Halmashauri ya Mji wa
Ifakara ili kuwapunguzia wananchi gharama ya kukodi gari kwa sh. 800,000 pale
wagonjwa wao wanapopata rufaa.
Wananchi wa Mji wa
Ifakara wameiomba Serikali iwasaidie kuwapatia gari la wagonjwa
kwani kitua chao hakina gari na wagonjwa wao wanapopata rufaa ya kwenda
hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Morogoro wanalazimika kukodi gari kutoka
hospitali ya Mtakatifu Francis kwa gharama ya sh. 800,000 ambazo baadhi yao
wanashindwa kuzimudi.
Waziri Mkuu ametoa
agizo hilo leo (Jumanne, Septemba 17, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa
Mji wa Ifakara katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa kituo cha
mabasi cha mji huo. Amesema iwapo fedha za makusanyo ya mapato ya
ndani katika halmashauri husika zingekuwa zinatumika vizuri
kusingekuwa na changamoto kama hizo.
Amesema Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imedhamiria
kuboresha huduma za afya kwa wananchi, hivyo amewataka wananchi hao kuendelea
kuwa na imani na Serikali yao. “Nitampigia simu Waziri Ummy (Wizara ya Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto) katika mgao ujao alete gari la
wagonjwa hapa.”
Pia, Waziri Mkuu
ameielekeza Ofisi ya Rais-TAMISEMI ihakikishe katika mgawo wa ujenzi wa
hospitali za wilaya, Halmashauri ya Mji wa Ifakara ipewe kipaumbele kwa sababu
eneo hilo ni kubwa na lina watu wengi lakini hakuna hospitali ya wilaya hivyo
kusababisha msongamano mkubwa katika kituo cha Afya cha Kibaoni.
“Nimetembelea
mwenyewe kituo cha Afya cha Kibaoni na nimeshuhudia msongamano wa wagonjwa,
mgao wa pili wa ujenzi wa hospitali za wilaya Mji wa Ifakara lazima upewe
kipaumbele. Suala la huduma za afya ni suala nyeti, hivyo ujenzi wa hospitali
hiyo ni muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi.”
Awali, Mganga
Mfawidhi wa Halmashauri ya Mji wa Ifakara, Dkt. Happyness Ndosi alisema kituo
cha Afya cha Kibaoni kinapokea na kuwahudumia wagonjwa wa nje 225
hadi 250 kwa siku na wagonjwa wanaolazwa ni kati ya 50 hadi 80 kwa siku.
Wakinamama wanaojifungulia kituoni hapo ni 400 kwa mwezi.
Akizungumzia kuhusu
changamoto zinazikabili kituo hicho amesema kina upungufu wa watumishi 92,
kwani kina jumla ya watumishi 83 huku mahitaji yakiwa ni watumishi
175, ukosefu wa gari la wagonjwa na pia hakina gari lolote la
kutolea huduma zikiwemo za chanjo, na usambazaji, uchakavu kwa baadhi ya
majengo kama la wagonjwa wa nje.
Pia, kituo
kinakabiliwa na ukosefu wa jengo la kutunzia watoto njiti, watoto wachanga na
wale wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kuzaliwa (neonatal unit), ufinyu wa
chumba cha kujifungulia pamoja na ukosefu wa mashine ya kutolea dawa za
usingizi (anesthesia machine).
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali haitokuwa na msamaha na
watendaji wa halmashauri watakaobainika kutafuna fedha za makusanyo ya mapato
ya ndani pamoja na fedha zinazotolewa kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa miradi
mbalimbali ya maendeleo kwenye maeneo yao.
“Fedha za mapato ya
ndani hazitumiki vizuri watu wanadukua mifumo, wanapaswa watambue kwamba
Serikali ipo makini wakati wote. Watumishi wote watakaobainika kujihusisha na
vitendo hivyo vya ubadhilifu hatua kali za kinidhami zitachukuliwa dhidi yao.
Watumishi wa umma mnatakiwa kutekeleza majukumu yenu kwa weledi.”
Waziri Mkuu amesema
watumishi wa umma wanatakiwa kujiepusha na migogoro kwa kuwa ni
kunyume na taratibu za kiutumishi. “Haiwezekani viongozi wakagombania zabuni
zitokanazo na fedha za kodi za wananchi, kwa ajili ya maslahi yao binafsi. Serikali
itasimamia zabuni zote.”
No comments:
Post a Comment