WAFANYABIASHARA MACHINGA COMPLEX JIJINI DAR ES SALAAM WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA - Wor'Out Media

Wor'Out Media is a premier site for selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the world. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.

Breaking

Tuesday, March 21, 2017

WAFANYABIASHARA MACHINGA COMPLEX JIJINI DAR ES SALAAM WATAKIWA KUZINGATIA SHERIA




WAFANYABIASHARA ndogondogo katika Soko la Machinga Complex Jijini Dar es Salaam wameshauriwa kubadilika na kuendesha shughuli zao kwa kuzingatia sheria badala ya kufanya biashara zao kimazoea.

Wito huo umetolewa leo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Simbachawene alipofanyaa ziara ya kikazi katika Soko hilo ili kusikiliza changamoto wanazokumbana nazo wafanyabiashara wa soko hilo.

“Nawapa pole sana ndugu zangu wafanyabiashara wa Machinga Complex mnaendesha biashara zenu bila kuzingatia sheria jambo linalo wagharimu hivi sasa katika biashara zenu leo nimekuja kuwarejesha kwenye mstari,” alisema Simbachawene.

Aidha Waziri Simbachawene amemuagiza Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam kuwachukulia hatua baadhi ya viongozi wa menejimenti ya Machinga Complex kwa kile kinachodaiwa utendaji wao mbovu na kujaza nadfasi zote zilizo wazi.

Wakati huohuo amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda kuteua Wajumbe wa Bodi ya Machinga Complex ili kuongeza ufanisi katika uendeshaji wa Soko hilo.

Pia Waziri Simbachawene ametoa wito kwa wafanyabiashara wote kulipa kodi zao kwa wakati huku hakitishia kuwaondoa katika vizimba (eneo la mraba la mauzo) wale wote watakao kaidi amri hiyo halali ya kulipa kodi kwa mujibu wa sheria na mikataba yao.

Awali akimkaribisha Waziri Simbachawene, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda amesema kuwa ujio wa Waziri huyo mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa imekuja wakati muafaka kwani ni takribani kipindi cha karibu mwaka mmoja tangu alipompa maagizo ya kushughulikia changamoto zinazokabili jengo la Machinga Complex kazi ambayo waliikamilisha na kukabidhi taarifa katika ofisi ya Waziri Simbachawene.

“Nidhahiri kuwa ziara yako Mhe. Waziri itatoa majawabu yatakayopelekea kutatua changamoto kadhaa zinazolikabili soko hili la Machinga Complex na ni imani yangu kwamba utatoa maagizo na kufanya maamuzi nasi hatuna budi ya kuyapokea na kutekeleza” alisisitiza Makonda.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam Bibi. Sipora Liana amesema kuwa changamoto kubwa inayokabili Soko hilo ni pamoja na deni linalokadiriwa kufikia zaidi ya shilingi bilioni 38 zianzodaiwa na Shirika la hifsdhi za Jamii (NSSF) ambao ndiyo waliojengwa majengo ya soko hilo linalomilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa changamoto nyingine inayokabili Soko hilo ni kutokuwapo kwa chombo cha maamuzi (Bodi) ambayo kazi yake kubwa ingekuwa kushughulikia changamoto zote za mradi huo.

Soko la Machinga Complex limejengwa kwa lengo la kutatua changamoto ya ukosekanaji wa soko la uhakika kwa wafanyabiashara wadogowadogo katika Jiji la Dar es Salaam ambapo ujenzi wake ulifanyika chini ya udhamini wa NSSF na kumilikiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam likiwa na uwezo wa kuchukua takribani wafanyabiashara 4206.

No comments:

Post a Comment

Sharing Buttons

Pages