Na Bakari Kimwanga -Aliyekuwa
Thailand
TAASISI mbalimbali za kimataifa zimekuwa na
mkakati madhubuti wa kulinda rasilimali hasa wanyama akiwamo kakakuona ambaye
kwa sasa yupo hatarini kutoweka.
Hali hiyo inachangiwa kwa kiasi kikubwa na
usafirishaji haramu wa wanyamapori kutokana nchi za Afrika hasa zile za Afrika
Magharibi zikiwamo Ghana na Nigeria, na kwa upande wa Afrika Mashariki Kenya
ikitajwa kama sehemu ya uchochoro wa ukusanyaji wa wanyama hao na kuwasafirisha
kwenda nchi za Asia.
Timu ya wanahabari watano kutoka nchini
ilitembela nchini Thailand na kuzunguka kwenye maeneo mbalimbali ikiwamo sehemu
maalumu za wanyama waliokamatwa kutoka nchi za Afrika, Idara ya Forodha Uwanja
wa Ndege wa Suvarnabhumi na soko la bidhaa ya wanyamapori.
Wanahabri hao waliungana na wenzao wa nchini
Thailand, ambapo kila upande uliweza kutembelea kwenye nchi za wenzake kwa
lengo la kubadilishana uzoefu na taarifa kuhusu usafirishaji haramu wa
wanyamapori, chini ya ufadhili wa USAID Protect Tanzania na USAID Wildlife
Asia, kwa kushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania
(JET).
Kutokana na hali hiyo, nchi ya Ghana
imelazimika kuingia katika mkakati wa kuangalia upya sheria zake za wanyamapori
kutokana na biashara ya kakakuona ambayo imekithiri kwa kasi kubwa.
Hali hii imesababishwa na hofu ya kwamba nchi
hiyo inatumiwa kuendesha biashara haramu.Zaidi ya kilo 31,000 ya magamba ya
kakakuona ilikamatwa duniani kote mwaka huu, hali hiyo inabainishwa na ripoti
ya Shirika la Kimataifa la Ustawi wa Wanyama (IFAW).
Katika kipindi cha Mei na Juni mwaka huu,
shehena mbili kubwa zilinaswa nchini Malaysia, ambapo pia kilo 700 zilipatikana
zikiwa zimesafirishwa kupitia Ghana. Huku shehena nyingine kubwa zikikamatwa
pia nchini Uganda, Cameron na Ivory Coast.
Mmoja wa maofisa wa juu wa IFAW, Mark Hofberg,
anasema magamba mengi kutoka kwa mnyama huyo Afrika yameuzwa ili kufikia
mahitaji yake katika Bara la Asia, ambako hutumiwa katika dawa za jadi.
Kakakuona anapatikana zaidi katika nchi za
Afrika na Kusini Mashariki mwa Asia.Aina mbili kati ya nane ya mnyama huyo
wameorodheshwa kuwa hatarini, wakiwekwa katika orodha nyekundu ya aina ya
wanyama walio hatarini.
“Kuongezeka kwa kamatakamata ya mizigo hiyo
kunaweza kuwa ishara kwamba mamlaka husika zinalichukulia suala hili kwa uzito,
lakini nchi nyingi hazina sheria kali za kuadhibu wafanyabiashara haramu.
“Kwa biashara hii kupungua kwa kiasi kikubwa,
kunahitajika adhabu na hukumu kali,” anasema Hofberg.Kakakuona ni mnyama
aliyehifadhiwa nchini Ghana, ambapo Mwenyekiti wa Tume ya Wanyamapori wa Ghana,
Nana Kofi Adu-Nsiah, anasema sheria kali inahitajika.
Sheria zilizopo za ulinzi wa wanyamapori
zilipitishwa katika miaka ya 1960 na tume hiyo inataka ziangaliwe upya ili
kufikia viwango vya kimataifa.Kutokana na ujangili huo mpya ambao sasa unashika
kasi, watu watatu walikamatwa nchini Ghana kuhusiana na mizigo iliyonaswa Juni,
mwaka huu, nchini Malaysia.
Viongozi wa Serikali wanaamini sheria mpya
zitazuia nchi za Afrika Magharibi kutumiwa kuwa hatua ya usafiri kwa wanyama
hao wanaosafirishwa lakini pia kuna wasiwasi pia juu ya uwindaji wa ndani wa
kakakuona.
Wanyama hao ambao wana ukubwa wa sentimita 30
hadi 100 wanaweza kuuzwa kwa karibu dola za Marekani 45 au Euro 38. Na wale
wanaowauza kwa kawaida huwa ni watu masikini.
UTAFITI
Watafiti wamegundua kuwa kakakuona anatumika
kwa ajili ya chakula na magamba yake yanatumiwa kama viungo.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na USAID
Wildlife Asia, uliainisha sababu za kuwapo kwa biashara haramu ya bidhaa za
wanyamapori kama tembo, faru, kakakuona na tiger kunatokana na imani na
tamaduni zao hasa kwa raia wa nchi za Thailand, China na Vietnam, ambapo pia
inaelezwa kuwa asilimia 20 ya tembo wa Afrika wanadaiwa kuuawa na sehemu ya
viungo vyao (pembe) husafirishwa kwa njia ya zisizo halali na kuingia kwenye
nchi hizo.
“Mtu anatoa zawadi iliyotengenezwa kwa mazao ya
wanyamapori kwa familia, marafiki, masuala ya kijamii na mitandao ya kibiashara
kwa mazao ya wanyama wote wanne,” anaeleza mtaalamu wa mawasiliano na
kubadilisha tabia wa USAID Wildlife Asia, Wenweena Tangsathianraphap.
Naye mfuatiliaji na mtaalamu wa uthamini na
ufuatiliaji USAID Wildlife Asia, Pakprim Oranop, anaweka wazi suala hili na
kusema kwamba bara hilo mtu kuvaa kidani au kitu chochote kilichotengenezwa kwa
kiungo chochote cha mnyama ni ishara kwamba naye atakuwa jasiri kama mnyama
aliyetokana na bidhaa hiyo au anajihakikishia ulinzi.
Hata hivyo, pia wapo wenye imani kwamba
inaongeza nguvu za kiume au uwezo wa mwanamume kutambulika kuwa rijali, na
wengine wakitumia kama dawa ya kuwafanya kuwa imara kama mnyama husika.
Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na USAID
Wildlife Asia, ya kwanini watu wanatumia bidhaa za wanyamapori, walibaini kuwa
kuna uhusiano wa moja kwa moja kati ya imani na utamaduni kwa wanaotumia bidhaa
za wanyamapori.
“Wengi waliamini kuwa anapotumia kitu chochote
kilichotengenezwa kwa jino la tembo, pembe ya faru au tiger (chui) basi naye
atakuwa na matendo ya kishujaa kama huyo mnyama, ndiyo maana wengi wameendelea
kutumia,” anaeleza.
Katika utafiti wa walaji wa mwaka 2018, kati ya
watu 10 waliohojiwa ambao ni wanunuaji na watumiaji kwa miezi 12 iliyopita,
ulibainisha kuwa nchini China watumiaji wa bidhaa za tembo asilimia 4.01 ni vya
tofauti, asilimia 3.86 waliamini katika imani za kiroho na asilimia 3.79
waliamini katika urembo.
Kwa upande wa kakakuona, asilimia 4.14
waliamini inaponya maradhi mbalimbali, 3.72 inaleta afya njema na maisha mazuri
na asilimia 2.74 inaongeza nguvu za kiume.
HALI
ILIVYO THAILAND
Asilimia 94 ya waliohojiwa nchin Thailand,
wanasema wanatumia bidhaa za meno ya tembo kwa kuwa ni kitu cha tofauti na
thamani kubwa, asilimia 88 wanasema inaleta matumaini na bahati, wakati
asilimia 79 wanasema inawalinda dhidi ya adui na majanga.
Kutokana na hali hiyo, Mwakilishi wa Shirika la
Kudhibiti Usafirishaji wa Wanyamapori Asia (Traffic), Monica Zavagli, anasema
biashara ya mazao ya wanyamapori inahusisha watu wenye mtandao mkubwa na wenye
fedha nyingi ambazo huzitumia kununua nyara hizo.
“Hii biashara ni kubwa ambayo inatumia zaidi ya
Dola za Marekani bilioni tisa hadi 30 kwa mwaka, mtandao huu unatumia taasisi
za kifedha kuhamisha fedha na benki zina uwezo wa kuchunguza kwamba fedha hizo
zinatokana na nini kama zinahusisha ujangili,” anasema.
“Hata hivyo, nchi kama Tanzania imefanya vizuri
kuwa na sheria kali, lakini jitihada zaidi zinahitajika katika kushirikisha
taasisi za fedha, kwa kufuatilia mali na mienendo yao kama fedha hizo
zinahusisha biashara hiyo itasaidia kumaliza mtandao huo,” anasema Monica.
Mkuu wa USAID Asia, Craig Karkpatrick, anasema
ripoti ya polisi wa kimataifa imeonyesha kuwa biashara haramu ya mazao ya
wanyamapori ipo na inafanyika kwa kiasi kikubwa.
HALI
ILIVYO TANZANIA
Kwa mujibu wa ripoti ya hali ya uchumi kwa
Taifa ya mwaka 2017, inaonesha kwamba sekta ndogo ya wanyamapori ilikusanya
zaidi ya Sh milioni 29 ikilinganishwa na zaidi ya Sh milioni 38 mwaka 2016,
sawa na upungufu wa asilimia 22.7.
Kati ya mapato hayo, mapato kwa sarafu ya ndani
yalikuwa Sh 2,904,631,101.82 na sarafu ya nje yalikuwa ni Dola za Marekani
11,940,029.80 ikilinganishwa na Sh 242,843,673,275 na Dola za Marekani
17,473,260 mwaka 2016.
Kwa mujibu wa Waziri wa Maliasili na Utalii,
Dk. Hamis Kingwangalla, Serikali inaendelea na jitihada za kulinda rasilimali
za wanyamapori dhidi ya ujangili na uvunaji usio endelevu.
Katika kipindi hicho, anasema kulikuwa na siku
za doria 262,770 zilizofanyika katika maeneo ya wazi na yaliyohifadhiwa
ikilinganishwa na siku za doria 518,809 zilizofanyika mwaka 2016.
NYARA
ZILIZOKAMATWA
Kutokana na doria hizo, nyara za Serikali za
aina mbalimbali zilikamatwa ambazo ni pamoja na meno ya tembo 296 yenye jumla
ya uzito wa kilo 929.8; nyamapori kilo 12,776; meno mawili ya simba, kakakuona
644; ngozi 10 za chui na ngozi moja ya simba.
Anasema pia jumla ya silaha 5,309 zilizohusika
katika ujangili zilikamatwa zikiwamo SMG tisa, hunting rifles 14, shotgun 56,
gobore 212, bastola mbili na nyaya za kutegea wanyama 5,016.
Huku watuhumiwa 3,889 wa makosa mbalimbali
yakiwamo ujangili nao walikamatwa na kesi zao kuamuliwa na waliopatikana na
hatia walilipa faini jumla ya Sh milioni 1.108 na wengine kufungwa jela miezi
12. Kesi 3,011 zilizobaki zilikuwa zinaendelea katika mahakama mbalimbali
nchini.
MSIMAMO
WA CITES
Katika mkutano wa wawakilishi wa nchi 183
wanachama wa mkataba wa kimataifa wa viumbe vilivyo hatarini kutoweka (CITES),
uliofanyika hivi karibuni Geneva, Uswisi kwa lengo la kuimarisha mikakati ya
kulinda viumbe hao, wanatoka na mapendekezo 56 yenye lengo la kuimarisha na
kulinda viumbe vya porini.
Katibu Mkuu wa CITES, Ivonne Higuero, anasema
tayari nchi hizo wanachama zimewasilisha mapendekezo 56 yenye lengo la kubadili
na hatimaye kuimarisha kanuni za kulinda viumbe vya porini wakiwamo wanyama
pamoja na maua, ambavyo vinauzwa kwenye soko la kimataifa.
“Mapendekezo mengi yanalenga kuhakikisha kuwa
viumbe hivyo vilivyoko hatarini na ambavyo vinaendelea kuuzwa, vinasalia
endelevu na hivyo mapendekezo yanataka vibali kutoka CITES ili kuruhusu
biashara yao,” anasema Higuero.
Anasema mapendekezo mengine yanataka kupigwa
marufuku kwa biashara za viumbe vilivyoko kwenye orodha I ilihali mengine
yanataka kuwa viumbe ambavyo tayari idadi yao imekaa sawa vihamishwe kutoka
orodha ya I kwenda orodha ya II ya mkataba wa CITES.
Anakumbusha kuwa kanuni zilizo wazi na
zinazotekelezeka kwa kuzingatia sera thabiti ni muhimu katika kulinda utajiri
wa asili na kufanikisha malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), ambayo
yalipitishwa na nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa mwaka 2015.
No comments:
Post a Comment