WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi saba
katika halmashauri mbili za wilaya ya Kilombero kwa tuhuma za ubadhilifu wa
fedha zaidi ya sh. bilioni 1.3 za makusanyo ya mapato ya ndani.Mbali na
kuwasimamisha kazi watumishi hao, pia Waziri Mkuu ameagiza watumishi hao
warejeshe fedha hizo ndani ya siku tatu kabla hajamaliza ziara yake ya kikazi
mkoani Morogoro. Watumishi hao ni Reina Mrema ambaye anadaiwa kuchukua kiasi
cha sh. milioni 298, Haile Njitango milioni 73, Linus Mdembo kiasi cha sh.
milioni 2 kwa kushirikiana na mtendaji huyo wa Kata.Waziri Mkuu amewasimamisha
kazi watumishi hao leo (Jumapili, Septemba 15, 2019) wakati akiongea na
watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero pamoja na watumishi wa
Halmashauri ya Mji wa Ifakara, akiwa katika siku ya pili za ziara yake ya
kikazi mkoani Morogoro.
Kuhusu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Ifakara Fransis
Ndulane ambaye aliingiziwa sh. milioni tano katika akaunti yake binafsi, Waziri
Mkuu ameagiza azirudishe mara moja na amkabidhi stakabadhi ya kuonesha kuwa
amerejesha fedha hizo kabla hajamaliza ziara yake mkoani hapa.
Amesema “Mkoa mzima wa Morogoro umekuwa na tatizo la upotevu
wa mapato, fedha zinakusanywa zinapita mikononi mwa watu hazifiki benki, hii ni
shida, hatutavumilia.”
Waziri Mkuu amesema kwa mujibu wa taarifa ya mkaguzi wa
hesabu za serikali (CAG) kipindi cha mwaka 2016 hadi juni 2019, Katika mji wa
Ifakara makusanyo yalikuwa ni bilioni 2.7 ambapo fedha iliopelekwa bank ni
shilingi bilioni 1.9 na kwamba kiasi cha shilingi milioni 727 hazijulikani
zilipoenda.
Amesema katika mitambo kumi ya ukusanyaji wa mapato
iliokaguliwa imeonyesha kiasi cha shilingi milioni 348 zilizokusanywa
hazikupelekwa bank na hivyo kuishia mikononi mwa watu.
Waziri Mkuu amesema katika uchunguzi huo ilibainika kuwa
fedha hizo ziliingizwa katika akaunti mbalimbali za watumishi wa halamshauri
hizo kutoka kwa mtendaji wa Kata ya Viwanja 60 katika Mji wa Ifakara aitwaye
Gregory Midas.
Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA
katika halmashauri ya Mji wa Ifakara, John Mvanga ambaye ndiye alibaini kuwepo
na ubadhilifu wa fedha hizo na badae kusimamishwa kazi, arejeshwe kazini mara
moja na asibugudhiwe.
“Mlimsimamisha kazi kwa sababu mlijua amegundua madudu yenu,
lakini haisaidi, arejeshwe kazini naagiza apewe ulizi wakutosha.”
Kwa upande wa Halmashauri ya wilaya ya Kilombero, Waziri Mkuu
amesema zaidi ya sh. milioni 600 hazijulikani zilipo huku kiasi cha shilingi
milioni 98.5 zikidaiwa kuingizwa katika akaunti za watumishi wa halamshauri
hiyo bila maelezo yeyote.
Waziri Mkuu amewataja watumishi hao kuwa ni Devid Onyango
aliyechukua kiasi cha milioni 51, Elakada Kanongole milioni 36, Fork Karunde
milioni 8 na Charlse Chali milioni 2.5.Amesema kati ya milioni hizo 600 kampuni
ya Kilombero Plantation LTD (KPL) ambao wanadaiwa kiasi cha shilingi milioni
531 ambazo hazikuingizwa katika mfumo huo.
No comments:
Post a Comment