Na: Sylvester Raphael
“Mipaka kati ya nchi moja na nyingine ni fursa ya kiuchumi kwa wananchi wanaoishi katika maeneo hayo wakifanya biashara kulingana na masoko yaliyopo katika nchi hizo. Wananchi wanaoishi katika mipaka wanatakiwa kutumia mipaka kufanya biashara na kutajirika kwa kufuata sheria za nchi na jukumu letu Serikali ni kuhakikisha wananchi hawa wananufaika na siyo kuwa kikwazo kwao na mipaka kuonekana si mahala pazuri pa kuishi.”
Msistizo huo ulitolewa na Profesa Faustine Kamuzora Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera wakati akitembelea mipaka ya Tanzania na Uganda iliyopo Mkoani Kagera Wilayani Missenyi (Kabindi- Kashenye, Mtukula na Bugango) pia Murongo Wilayani Kyerwa Januari 22 hadi 23, 2019 alipokutana na wananchi na watumishi katika mipaka hiyo ili kuona namna bora ya wananchi wanaoishi mipakani wanavyoweza kunufaika na mipaka hiyo huku Serikali ikiwawekea mazingira mazuri ya kibiashara.
Hii ni kutokana na uongozi wa Mkoa wa Kagera kuweka azma ya mwaka 2019 kuwa mwaka wa kodi kwa wafanyabiashara wote wakubwa na wadogo kuhakikisha wanalipa kodi stahiki na rafiki ambayo itawafanya kuendelea kufanya biashara zao na kunufaika. Katika hali hyo Profesa Kamuzora anasema lazima Serikali kuyajua matatizo wanayokumbana nayo wafanyabiashara na kuyafanyia kazi ili wananchi wanufaike na fursa zilizopo katika mazingira yao.
Mara baada ya kutembelea Mwalo wa Kabindi Kashenye Wilayani Missenyi mpakani mwa Tanzania na Uganda upande wa Ziwa Victoria na kuongea na wananchi wa Mwalo huo ambao ni wavuvi walimweleza Profesa Kamuzora kuwa kuna shida ya soko la samaki wakati mwingine viwanda vilivyopo Bukoba vinapata samaki wa kutosha na havinunui samaki wao jambo ambalo linawatia hasara au kulazimika kuuza samaki kwa bei ndogo wakati katika nchi jirani ya Uganda kuna soko zuri la samaki na kwa bei nzuri lakini hawaruhusiwi kuuza huko.
Profesa Kamuzora baada ya kusikilza kilio chao aliwaeleza kuwa ndiyo maana alimua kutembelea mipaka ili aone changamoto zilizopo ili Serikali iweze kuzifanyia kazi ambapo alisisitiza kuwa maana ya kuwa mpakani unatakiwa kucheza na fursa za nchi zote mbili ili utajirike. Profesa Kamuzora aliwaeleza wavuvi hao kuwa Serikali itaangalia namna bora ya kuona nchi jirani Uganda kama kuna bei nzuri ya samaki wavuvi waruhusiwe kuuza huko kwa kufuata sheria na kulipa ushuru wa Serikali lakini pia kutoa changamoto katika viwanda vya ndani ili vitoe bei nzuri kwa wavuvi.
Pia Profesa Kamuzora alisisitiza kuwa wananchi wanaokaa mipakani wanatakiwa kunufaika na mipaka hiyo kwani likitokea jambo baya mfano vita au magonjwa wao ndiyo wa kwanza kudhurika tofauti na katikati mwa nchi kwa hiyo ni vizuri hata fursa za biashara ziwanufaishe kwani wananchi hao ni ndugu bali mipaka iliwekwa tu Wakoloni lakini bado wao wana mahusiano makubwa.
Katika hatua nyingine Profesa Kamuzora alimuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi kupima viwanja haraka iwezekanavyo katika eneo la Kabindi Kashenye ili kuwe na mji uliopangika na wananchi hasa wanaojihusisha na uvuvi katika eneo hilo waweze kuwa na makazi bora lakini pia na wawekezaji ambao wangependa kuwekeza katika eneo hilo wakute viwanja vilivyopimwa ili paweze kuchangamka kama upande wa pili wa nchi jirani Kasensero.
Profesa Kamuzora akiwa katika mpaka wa Mtukula ambapo alipata fursa kuongea na watumishi wa idara zote za Serikali zinaotoa huduma katika mpaka huo aliwaeleza watumishi hao kuwa wanatakiwa kutokuwa kikwazo kwa wananchi wanaojishughulisha na biashara katika mpaka huo bali wawe wabunifu katika kazi zao na kutekeleza sheria lakini wakiongozwa na busara kubwa katika kutatua changamoto mbalimbali za kuwasaidia wananchi kutumia fursa ya mpaka kufanya biashara.
“Sisi watumishi wa umma tusiwe kikwazo kwa watu wetu kuwa mpakani ni fursa kubwa ya wananchi wetu kutajirika, ukienda nchi nyingine wananchi wa mipakani ndiyo matajiri kwasababu wamepewa fursa ya kufanya biashara katika pande zote mbili lakini kwa kuzingatia matakwa ya sheria. Sisi tuwe mwangaza na njia kwao badala ya kuwa vikwazo ili tuinue uchumi wao.” Aliwaasa watumishi wa Mtukula Profesa Kamuzora
Aidha, Profesa Kamuzora alisema kuwa baada ya kutembelea mipaka hasa Mtukula, Bugango na Murongo changamoto kubwa aliyoiona ni upande wa pili wa nchi jirani Uganda wafanyabiashara kuchangamkia fursa karibu na mipaka kwa kuanzisha miji na vituo vya biashara wakati huku upande wa Tanzania kukiwa hakuna kilichoendelezwa na kupelekea Watanzania kunufaisha wenzao wa nchi jirani kwa kununua bidhaa huko.
Profesa Kamuzora anasema kuwa kunatakiwa kufanyanyika upembuzi wa kina kuona kwanini nchi jirani wanatambua fursa za mipaka lakini sisi upande wa Tanzania bado. Mfano Mtukula maduka ya bidhaa mbalimbali yapo upande wa pili wakati huku Tanzania hakuna, hivyo hivyo Bugango Waganda wana maduka makubwa ya bidhaa lakini Tanzania hakuna na Murongo upande wa Uganda Kikagati kuna mji wa kibiashara lakini Tanzania hakuna, mipaka yote Watanzania wanavuka kutafuta manunuzi nchi jirani.
Profesa Kamzora akiongea na watumishi na Viongozi mbalimbali katika Wilaya hizo mbili za Missenyi na Kyerwa alisema kuwa kuna haja ya Serikali kuangalia upya mifumo ya kodi pia kufanya utafiti kwanini wenzetu wanapata fursa ya kufungua biashara mipakani lakini Watanzania hawafanyi hivyo wakati mwingine wanakwenda kufungua biashara upande wa nchi jirani lakini si upande wa Tanzania.
Baadhi ya wafanyabiashara wa mipakani aliokutana nao Profesa Kamuzora walimweleza kuwa upande wa nchi jirani Uganda kodi zao ni nafuu katika kufungua biashara ukilinganisha na Tanzania na ndiyo maana maduka na biashara zianaanzishwa upande wa pili kuliko upande wa Tanzania. Pia walimweleza kuwa katika upande wa Tanzania mipakani Miundombinu kama umeme maji na pengine barabara nzuri za rami zilicheleweshwa kufika katika mipaka hiyo jambo ambalo linakwamisha sana kibiashara.
Vilevile wafanyabisaha walimweleza Profesa kamuzora kuwa upande Tanzania kuna mamlaka nyingi ambazo zinasimamia sheria zinazofanana na kuleta usumbufu mkubwa kwao mfano TFDA, TBS na nyinginezo ambazo kama zingepunguzwa au kuunganishwa majukumu yake ingeweza kuondoa usumbufu na Watanzania wakaweza kufungua au kuwekeza kibiashara katika upande wa Tanzania.
Profesa Kamuzora aliwashauri viongozi na Watendaji wa Halmashauri za Wilaya zilizopo mipakani kuona namna bora ya kuzibaini na kuzichambua chanagamoto mbalimbali zilizopo mipakani na kuishauri Serikali kwani wao ndiyo wanaishi katika maeneo husika kuliko viongozi waliopo Dodoma na Dar es Saam ili changamoto hizo zifanyiwe kazi kulingana na uhalisia.
“Mimi nashauri Mkuu wa Wilaya Pamoja na Wakurugenzi mliopo mipakani kukaa chini na kuzichambua changamoto hizi na kutuletea Mkoani ili nasi tuzipeke mahali panapohusika Serikali ni sikivu itazifanyia kazi. Mfano huwezi kuelewa mpaka ufike huku hata mimi nikiwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu nilikuwa napokea mengi lakini baada ya kufika huku na kujionea ndiyo nimeelewa zaidi. Ibueni nyinyi tuleteeni mkoani ili tuyasukume ili sheria zifanye kazi kulingana uhalisia.” Profesa Kamuzora alisistiza
Profesa Faustine Kamuzora aliyeteuliwa na Rais John Pombe Magufuli kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera tarehe 8 Januari, 2019 na kuapishwa Januari 9, 2019 aidha, aliripoti Mkoani Kagera tarehe 10, Januari, 2019 anasema baada ya kukabidhi ofisi sasa ameanza kazi rasmi Mkoani Kagera lakini akianza na kujifunza kwa kupitia mipaka na kuona changamoto zake na kuona namna bora ya kuweka ustawi wa wananchi katika kufanya biashara zao bila bughudha.
No comments:
Post a Comment