Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imetakiwa kufanya ufuatiliaji wa utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu katika taasisi zote za umma kwa lengo la kuondoa tatizo la uvujaji wa siri za serikali.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) wakati akizungumza na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo jijini Dodoma, yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya idara hiyo na kujiridhisha namna idara hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesema, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ndiyo inayohusika na masuala yote ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka hivyo inatakiwa ijiwekee utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa namna ya nyaraka zinavyotunzwa na kushauri namna bora ya utunzaji wa nyaraka hizo.
“Tujenge tabia ya kufanya ufuatiliaji wa Miongozo tunayoitoa ili kuona kama inatekelezwa inavyotakiwa kwani tusipofanya hivyo taasisi zinafanya inavyotaka na matokeo yake ni kuvuja kwa siri za serikali,” Mhe. Dkt. Mwanjelwa amesisitiza.
Mhe. Dkt. Mwanjelwa amemtaka Mkurugenzi wa idara hiyo kuwa mkali na kuchukua hatua za kinidhamu kwa taasisi zote za umma zinazoshindwa kutekeleza ipasavyo jukumu la utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka na hatimaye kusababisha siri za serikali kuvuja.
Aidha, Mhe. Dkt. Mwanjelwa ameipongeza idara hiyo kwa kutumia njia za kisasa za TEHAMA katika kutunza kumbukumbu na nyaraka na kuwataka kuongeza kasi ya kuzihifadhi nyaraka hizo kidigitali ili kuimarisha usalama wake.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi ameyataja majukumu ya idara yake kuwa ni pamoja na kuweka mifumo ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka katika taasisi za umma, kutoa ushauri juu ya utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka na kuratibu mipango ya kutunza na kuhifadhi kumbukumbu muhimu katika taasisi za umma, kuweka na kusimamia viwango vya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika taasisi za umma.
Bw. Msiangi ameendelea kutaja majukumu mengine kuwa ni kukusanya na kuhifadhi nyaraka zenye umuhimu kitaifa ili kulinda urithi andishi wa nchi yetu, kuandaa na kusimamia utekelezaji wa Miongozo ya kutunza na kuteketeza kumbukumbu katika taasisi za umma, kufanya tathmini ya kumbukumbu tuli (majalada yaliyofungwa) ili kutambua majalada yenye umuhimi wa kudumu kwa ajili ya kuyahifadhi, kuhifadhi nyaraka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji na kulinda nakala halisi na kukusanya, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za vitu vya Waasisi wa Taifa.
Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ilianza kutekeleza majukumu yake kama idara inayojitegemea kuanzia mwezi Julai, 2015 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa Awamu ya Nne kupitisha muundo wa Idara tarehe 12 Februari, 2015. Hata hivyo idara hii inaanzia mwaka 1963 wakati Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipotoa Waraka Na.7 wa Mwaka 1963 ulioelekeza kutunza, kuhifadhi na kuteketeza nyaraka za Serikali.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akipata ufafanuzi kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi kuhusu mifumo ya TEHAMA inavyofanya kazi katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji katika idara hiyo jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akishiriki kutoa nakala ya nyaraka ili kuihifadhi katika mfumo wa TEHAMA alipofanya ziara ya kikazi katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji. Anayemsaidia kutoa ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akishuhudia baadhi ya kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa katika majalada kwa ajili ya rejea ya kiofisi alipofanya ziara ya kikazi katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akipata maelezo kutoka kwa Mtunza Kumbukumbu Msaidizi, Bi. Joyce Maro juu ya kumbukumbu zilizohifadhiwa katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya kikazi katika Idara hiyo kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akisisitiza namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za serikali ili kuondokana na tatizo la uvujaji wa siri za serikali alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Dkt. Mary Mwanjelwa (Mb) akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji katika idara hiyo jijini Dodoma.
No comments:
Post a Comment